Na Ashrack Miraji Matukio Daima App
Nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa jana alipokutana na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam. Katika hotuba hiyo, Rais alizungumzia masuala mbalimbali muhimu kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu.
Tumemsikia na tumemwelewa vyema. Ameendelea kutupa mwanga sisi kama Watanzania na kutuondolea wasiwasi katika mambo kadhaa yanayohusu mwenendo wa nchi yetu. Aidha, aligusia changamoto mbalimbali zilizopo duniani na kutoa msimamo wa Serikali kwa maslahi ya Taifa.
Hakuna kiongozi yeyote duniani anayependa kuona wananchi wake wanaishi kwa hofu na hali ya wasiwasi itakayowafanya washindwe kutekeleza shughuli zao za kila siku. Kila kiongozi hutamani wananchi wake waishi kwa amani, upendo na utulivu. Hata maandiko ya vitabu vya dini yanasisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na kujiepusha na uvunjifu wa hali hiyo.
Nichukue fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake nzito. Kama mama mlezi wa Taifa, alitoa pia onyo kwa vijana kuheshimu sheria za nchi. Baadhi ya vijana wamekuwa wakitumiwa na watu wachache wanaoishi nje ya nchi kwa ajili ya propaganda zinazoweza kuhatarisha utulivu wa Taifa.
Natoa rai kwa wazee waliokuwepo na wale ambao hawakufika kwenye kikao hicho kuzungumza na watoto na wajukuu wao. Ni muhimu kuhakikisha kuwa hawadanganywi na watu wanaotumia mitandao kuhamasisha vitendo visivyokuwa na tija kwa Taifa. Kama msemo unavyosema, “Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu”. Kwa mantiki hiyo, vijana wanapaswa kujielimisha na kutokuwa rahisi kutumika vibaya.
Ni vyema tukakumbuka kuwa tuna Jeshi la Polisi lenye jukumu la kulinda usalama na mali za wananchi. Hivyo, nawashauri vijana na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu tarehe 9, waendelee na shughuli zao kama kawaida na wahakikishe amani inatangulizwa mbele.
Natoa pia wito kwa viongozi wa dini waliopewa wajibu wa kuhubiri neno la Mungu. Mungu amewatumia kueneza injili, si kuendesha masuala ya kisiasa ambayo yanaweza kuleta mpasuko katika jamii. Taifa linahitaji amani, upendo na utulivu. Hivyo, ni muhimu viongozi wa dini kusimamia wajibu wao na kuepuka kutumiwa vibaya. Taifa letu linaongozwa kwa mujibu wa sheria, na tunapaswa sote kuliheshimu hilo.






0 Comments