Header Ads Widget

JAMBO AWANYOOSHEA VIDOLE WATUMISHI WAZEMBE MEATU.

 

MBUNGE wa Jimbo la Meatu, Salum Khamis (Jambo) akizungumza kwenye kikao cha kuapishwa Madiwani kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu.


Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.


MBUNGE wa Jimbo la Meatu, Salum Khamis (Jambo), amewataka Watendaji wa serikali wilayani Meatu Mkoani Simiyu, kufanya kazi kwa bidii hasa kutatua kero za Wananchi kwani kazi iliyopo mbele ya viongozi wa kuchaguliwa ni kubwa kuliko suala la uchaguzi.


Amesema kuwa wananchi Wana matumaini makubwa na viongozi wa kuchaguliwa ikiwemo Wabunge na Madiwani, hivyo Watendaji wanapaswa kutatua changamoto za wananchi ambazo wamezieleza wakati wakutafuta kura.





Akizungumza kwenye kikao cha kuapishwa Madiwani, kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Meatu, Jambo amewataka watumishi hao kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.



"Tuna kazi kubwa kuhakikisha wananchi wanapata walichokitumaini kwetu, watendaji Mbadillike, ile Biashara ya kawaida muiache...Yaliyotokea nyuma hatutaki kuyaona yakijirudia, wananchi wetu vijijini hawahitaji mambo makubwa, wanachohitaji ni mahitaji yao ya msingi" amesema na kuongeza.


" Wananchi wetu wako hapa wametutuma kuwaletea Maendeleo, vijijini wamewekeza nguvu zao, haiwezekani na haitawezekana ndani ya miaka mitano wamechangishana hela kujenga boma usawa wa lenta na hakuna kilichoendelea...kwangu mimi haitowezekana, kuna mahala nilitoa mabati miaka mitano mpaka leo hayajatumika"


Jambo amesema kuwa amegombea nafasi ya Ubunge ili kusaidiana kutatua changamoto za wananchi, hivyo anatarajia watumishi kufanya kazi kwa weledi na wale ambao hawajitumi waachie ngazi.


"Haitawekana na haitowezekana, tutasambaratishana awamu hii, kwa mfano, zahanati ya Mwanjolo imekamilika na imesajiliwa lakini haijafunguliwa sababu ya kukosa kiti na meza mwaka mzima sasa...fedha za miradi ya Maendeleo ni kodi ya wananchi, zisimamieni" amesisitiza.


Aidha Jambo amesema kuwa atahakikisha anatekeleza ahadi alizotoa wakati wa kuomba kura haijalishi zinatekelezwa kwa gharama Gani huku akisisitiza kuwa kuna Ilani ya CCM na Ilani ya Jambo katika Jimbo la Meatu.


Amesema kuwa atahakikisha wataweka uwiano wa kutekeleza shughuli za Halmashauri Kuu, serikali na Jambo amefanya nini katika kuwatumikia wananchi hasa changamoto ya Maji ambayo wameipatia ufumbuzi wa muda mfupi sasa na pia wamepata suluhisho la tatizo la Maji kupitia Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria.


Katika hatua nyingine, Jambo amesema kuwa nchi ipo kwenye taharuki na kwamba kuna watu Wana dhamira ya kutuharibia nchi ambapo wilaya ya Meatu hawahusiani na matatizo hayo. 


"Meatu tusikubali kuvurugwa na maneno yasiyo na msingi, unayemsikia anataka kuvunja amani, toeni ripoti...Wenyewe tufanye ulinzi wa Wilaya na familia zeetu, tuhakikishe tunalinda nchi yetu" amesema.


Mwisho.













Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI