Na. Philipo Hassan / Mahale
Historia fupi ya Carter:
Carter ni mmoja wa Sokwe wakongwe wanaopatikana ndani ya Hifadhi ya Taifa Milima Mahale, akiwa na umri wa miaka 40. Sokwe huyo ni mtoto wa sokwe jike maarufu kwa jina la Calliope, aliyefariki mwaka 2009 akiwa na miaka 51.
Carter alikuwa na ndugu wawili, wa kiume mmoja; aitwaye Cadmas, alifariki mwaka 2010 akiwa na miaka 18 baada ya kushambuliwa na aliekuwa kiongozi wa kundi wakati huo (Alpha Male) aitwaye Pimu, na ndugu wa kike mmoja aitwaye Carmen ambapo Carmen alihama kundi baada ya kutimiza umri wa miaka 11.
Sokwe Carter amezeeka na sasa ni babu mlezi, mtulivu, mwema na anapenda kukaa karibu zaidi na watoto kuliko madume wenye nguvu wanaoongoza kundi lake la Sokwe wa Mahale.
Wakati nyingi huonekana akitembea kwa utulivu ndani ya kundi kubwa la sokwe, akifurahia maisha ya amani anayoyaishi na jamii ya kundi lake. Na nyakati zingine hupendelea kupata utulivu wa kujitenga na vurugu ambazo husababishwa na madume wa kundi lake.
Kwenye video hii, Carter anaonekana akicheza na mtoto wa miaka 4, jambo ambalo limekuwa sehemu ya tabia yake ya kila siku.
Pia hupenda kukaa na watoto, kuwatazama, na kucheza nao huku akitengeneza uhusiano wa kipekee unaowafanya watoto kumpenda na kumfuata kila mara.
Madume wengi wa Sokwe katika umri wa kati ya miaka 20 na 30 huepuka sana kucheza na Watoto sababu ya kuhofia kutoheshimiwa na watoto katika jamii ya koo zao.
Uongozi katika Ukoo wake:
Ingawa ni dume aliyewahi kufika nafasi ya 5 katika uongozi wa ukoo wake, hajawahi kufika uongozi wa juu. Tangu akiwa kijana, Carter hajawahi kupenda mabishano, makabiliano au misuguano.
Sokwe huyo hapendi ugomvi kabisa, hali iliyosababisha hadi leo kutokuwa na majeraha makubwa katika mwili wake ishara kuwa maisha yake amekuwa akiepuka migogoro.
Kitu pekee unachoweza kuona kwa Carter ni makovu ya michubuko michache tu ambayo aliipata akiwa na umri wa miaka 30 katika jitihada zake za kupambania sokwe jike wakiwa katika kipindi cha kupandwa.
Tabia yake kijamii:
Nyakati pekee ambazo Carter huonyesha msimamo mkali ni pale anapozungukwa na kundi la majike watupu, ambapo hutoa ishara ya kuunguruma kama utambulisho wa uwezo wake, bila kuanzisha vita wala kumuumiza yeyote na baadae hutulia akiona dume mwingine amesogea eneo alipo.
Hali hiyo humsaidia sana kuweza kupata majike pindi yanapokuwa kwenye joto. Dume hufanya vurugu kwa majike wakiwa katika hali ya kawaida jambo ambalo humsaidia kufanikisha kuwapata majike kirahisi wakiwa kwenye hali ya joto.
Kwasasa Carter Ndio Sokwe Dume mwenye umri mkubwa kuliko madume wote walioko kundi la Sokwe wa Mahale. Sokwe hufikia umri wa miaka 50 hadi 55 wakiwa mazingira yao asilia (msituni) na umri wa zaidi ya miaka 60 wakiwa maeneo ya bustani za wanyama.
Kwasasa Sokwe mwenye umri mkubwa kuliko wote Duniani ni Sokwe aitwae Joao mwenye umri wa Miaka 81, anaeishi kwenye Bustani ya Sokwe “Chimp Eden” iliyopo nchini Afrika Kusini.
Sokwe wa Mahale ni hazina ya utalii ambayo inaleta mapato kwa Taifa, inaimarisha uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi na kuongeza ajira kwa Watanzania. Kwa kuhakikisha usalama wao leo, tunalinda urithi wa kisayansi, kitamaduni na kiuchumi utakaoendelea kunufaisha kizazi hiki na kijacho.










0 Comments