Header Ads Widget

MALINYI NA ULANGA ZACHAGULIWA KULIMA ZAO LA KOROSHO KWA MALENGO




Na Lilian Kasenene, Morogoro

Matukio DaimaApp 


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam  Malima, amesema mkoa huo umekuja na mkakati mpya wa kuendeleza zao la korosho, ambapo Halmashauri za Malinyi na Ulanga zimechaguliwa kulimwa zao hilo kwa lengo la kuziendeleza wilaya hizo na kuwawezesha wananchi kuongeza vipato vyao.


Alibainisha hayo  wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Morogoro.



Malima alisema, licha ya Mkoa wa Morogoro kuwa na mkakati wa mazao yatakayowainua wananchi kiuchumi na kutunza mazingira, mkoa pia umeendelea kutambua na kuanzisha mazao mapya, ambapo zao la korosho limepangwa kustawishwa katika Halmashauri za Malinyi na Ulanga ili kuziendeleza na kukuza uchumi wa wananchi wake Mkoa na Taifa.


“Tumekubaliana kuwa korosho ni zao jipya la Mkoa wa Morogoro. Tuna mazao kama manne au matano, lakini moja muhimu ni korosho. Wameniuliza nipeleke wapi korosho, nikawaambia pelekeni Malinyi na Ulanga,” amesema Adam Malima.


Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alimtaka Meya wa Manispaa ya Morogoro Khalid Matengo  kuhakikisha anasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha Halmashauri hiyo kuwa na sifa na kufikia hadhi ya kuwa jiji.


Akawapongeza wenyeviti wa halmashauri za mkoa huo kwa kuchaguliwa kuongoza halmashauri na kuwataka  kufanya kazi kwa ushirikiano, na kuwasisitiza kuacha majungu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.


Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa amekwrwa na tabia ya baadhi ya Wabunge hasa wa majimbo kushindwa kuhudhulia kikao Cha ushauri Cha mkoa Rcc.


Malima alisema "Wapo baadhi ya Wabunge wamekuwa hawahidhulii vikao vya ushauri vya Wilaya na mkoa vya kujadili Maendeleo,".


Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Mecktridis Mdaku  akizungumzia  sekta ya kilimo katika wilaya hiyo alisema moja ya ajenda iliyopo ni kuendeleza mazao ya kimkakati  ikiwemo zao la korosho, ufuta na kakao .



“Sisi kwa wilaya ya Malinyi tumehamasisha kwa kiwango kikubwa  wakulima kulima zao la mkakati la korosho, japo wapo wachache wameanza kulima zao hilo, isipo kuwa wengine bado kutokana na kujenga mazoea ya kulima mpunga, inabidi tuzidi kuwapa elimu , tuwahamasishe wajue kwamba korosho nalo pia ni zao la kibiashara”alisema Mdaku.


Mbunge wa Jimbo hilo alisema endapo wananchi wa wilaya hiyo wanaongeza bidii ya kulima zao la korosho  pia wataondokana na umaskini ikiwa na kukuza uchumi kwa wilaya ya Malinyi


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI