FARIDA MANGUBE, MATUKIO DAIMA APP MOROGORO
Serikali imezitaka kampuni zinazojihusisha na uchimbaji wa madini mkakati ya graphite kuhakikisha zinazingatia kikamilifu utunzaji wa mazingira na uwajibikaji kwa jamii.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati wa ziara yake katika mradi wa Synergy Tanzania Company Ltd uliopo Wilaya ya Morogoro.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa amepongeza kuanza kwa uzalishaji wa madini hayo muhimu kwa teknolojia ya kisasa, huku akisisitiza umuhimu wa kumbukumbu sahihi za uzalishaji, ajira na miradi ya kijamii.
“Nachukua fursa hii kuwapongeza kwa hatua mliyofikia ya kuanza uzalishaji wa madini haya muhimu katika teknolojia ya kisasa. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha mnatunza mazingira ipasavyo na kuwasilisha mpango wa ulinzi wa mazingira kama inavyotakiwa kisheria,” amesema Dkt. Kiruswa.
Katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa pia ametembelea mgodi wa Yusra Yusufu unaoshirikiana na kampuni ya Guanui Mining Investment Group Ltd kukata mawe ya Maruru uliopo katika kijiji cha Mkuyuni, Wilaya ya Morogoro, ambapo ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji wake mkubwa unaochangia ukuaji wa uchumi, huku soko la bidhaa zake likiwa ndani na nje ya nchi.
Sambamba na hilo, Naibu Waziri amekutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, ambaye ameahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Madini pamoja na Ofisi ya Madini Mkoa wa Morogoro ili kuongeza ufanisi na udhibiti wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Zabibu Napacho, amesema Ofisi ya Madini Morogoro inaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali za Mitaa, Manispaa na Halmashauri za Wilaya na vijiji kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa madini na upatikanaji wa taarifa sahihi za shughuli za sekta ya madini.
Naye, Meneja wa Kampuni ya Synergy Tanzania Company Ltd, Sanjay Dabhi, amesema kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi zaidi ya 120 wa kudumu na wafanyakazi 66 wa muda mfupi. Ameongeza kuwa kampuni hiyo inashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya uwajibikaji kwa jamii zinazozunguka eneo la mradi.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Madini ya Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kupata taarifa za kina kuhusu shughuli za madini katika mkoa huo, ambapo alipata pia fursa ya kuzungumza na watumishi wa ofisi ya madini wa mkoa huo.

.jpeg)


.jpeg)


.jpeg)




0 Comments