Header Ads Widget

DIT WAAGIZWA KUANDAA UTARATIBU WA KUWAPELEKA WANAFUNZI NJE YA NCHI.

  Na Mwandishi Wetu.

Serikali imeiagiza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuandaa taarifa maalum itakayowezesha utekelezaji wa mpango wa kupeleka wanafunzi nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo na kupata ujuzi zaidi. 


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametoa maelekezo hayo wakati wa mahafali ya 19 duru ya kwanza ya DIT yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Desemba 05 , 2025.

“Taarifa hii ni muhimu ili serikali ijue bajeti halisi ya kuwawezesha wanafunzi kwenda kujifunza nje na kurejea wakiwa na ujuzi unaowawezesha kuajirika au kujiajiri,” amesema Prof. Mkenda.

Aidha, Waziri Mkenda amesema serikali inatarajia kuzungumza na Ubalozi wa China ili ufadhili wa masomo kwa vyuo vya nchi hiyo uingizwe chini ya mpango wa Sandwich, hususan kwa wanafunzi wa kozi za uhandisi. Amefafanua kuwa DIT tayari ina makubaliano ya ushirikiano wa kielimu na taasisi za China yanayowawezesha wanafunzi kusoma ngazi ya Diploma nchini humo na kurejea nchini kukamilisha shahada. “Mpango wa Sandwich unawawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika kampuni za ndani na nje ya nchi,” ameongeza.

Katika kuboresha elimu kwa vijana, Profesa Mkenda amesema Wizara itatenga fedha kupitia utaratibu wa Samia Scholarship ili kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutoa elimu yenye ujuzi na kuongeza ajira.

 “Leteni taarifa ya bajeti ili tujue mwanafunzi anahitaji nini ili fursa hizi zizidi kuwafaidisha” amesema Waziri huyo akiwahimiza wahitimu kuendelea kujifunza na kupanua maarifa.

Waziri Mkenda amebainisha kuwa kuanzia mwaka 2026, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita wataanza kunufaika na mpango wa kujifunza nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi, Mhandisi Dkt. Richard Masika, amewahimiza wahitimu kutumia ujuzi walioupata kwa vitendo akisema, “Elimu bila matendo ni sawa na mti bila matunda.” Amewahimiza kuongeza ubunifu, nidhamu na bidii ili kuendana na mahitaji ya dunia ya sasa ambayo inahitaji wataalam wabunifu na wenye kutatua changamoto.

Naye Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Profesa Preksedis Ndomba, amesema DIT imeendelea kupanua ushirikiano na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, ambapo hadi sasa imesaini makubaliano na zaidi ya taasisi 50. Amesema makubaliano hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi na walimu kwa kuwawezesha kupata fursa za kujifunza, kuongeza ujuzi na kubadilishana uzoefu.






















Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI