Header Ads Widget

WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI SIMIYU WAPAZA SAUTI: “TUNAWEZA TUKIPEWA UMEME NA MIKOPO”


WACHIMBAJI Wadogo wa Madini wa Mkoa wa Simiyu wameiomba Serikali pamoja na taasisi za kifedha kuwaunga mkono kwa kuwapatia umeme wa kudumu na mikopo yenye masharti nafuu, wakisema changamoto hizo zimekuwa kikwazo kikubwa katika kuongeza uzalishaji wa madini, hususan dhahabu.

Mmoja wa wachimbaji wanawake kupitia Chama cha Wachimba Madini Wanawake Tanzania (TAWOMA) mkoani humo, Anisia Japhet, amesema wamekuwa wakitumia gharama kubwa kuendesha mitambo kutokana na kutegemea nishati ya dizeli.

“Tunatumia dizeli ambayo ni ghali. Lita 80 zinamalizika ndani ya saa 24. Tungepata umeme wa kudumu, tungepunguza gharama na kuongeza tija,” amesema Anisia.


Ameongeza kuwa uchimbaji si kazi ya wanaume pekee bali ni fursa yenye manufaa makubwa kwa wanawake wanaojituma.

“Nikiwa mwanamke, nimefanikiwa kusomesha watoto na kuendesha maisha yangu kupitia uchimbaji. Kila mwezi tunapata wastani wa viroba 100 vya mawe, na kila kiroba kinaweza kutoa gramu moja au zaidi za dhahabu,” ameongeza.

Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi wa TAWOMA, Paul Ntalima, amesema wanamiliki maduara 24 ya uzalishaji, lakini ni maduara 14 pekee yanayoendelea na kazi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.


“Wachimbaji wadogo wana uwezo wa kuongeza tija mara mbili zaidi endapo watapatiwa mikopo yenye riba nafuu. Tunatengeneza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya 400. Sekta hii si tu inaleta kipato, bali pia inaimarisha maisha ya wananchi. Tukipata umeme wa gridi, uzalishaji utaongezeka mara mbili hadi tatu,” amesema Ntalima.

Naye Mussa Kazidijshi, Mtendaji wa Mgodi wa Ludovic Mlalo & Partners, amesema mgodi wao unaajiri zaidi ya wafanyakazi 200 na umeendelea kurejesha kwa jamii kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara.

“Jamii inanufaika hasa wakati wa mvua ambapo barabara huboreshwa na milipuko ya magonjwa hupungua. Tukipatiwa mikopo ya riba nafuu na nishati ya kudumu ya umeme, uzalishaji wetu utaongezeka mara tatu,” amesema Kazidijshi.


Akizungumzia changamoto hizo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Simiyu, Mayigi Makolobela, amesema Serikali kupitia Tume ya Madini kwa kushirikiana na TANESCO inaendelea na mazungumzo kuhakikisha maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani humo yanapatiwa umeme wa kudumu.

“TANESCO wameahidi kufikisha umeme katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo mkoani Simiyu ili kuongeza uzalishaji na kupunguza gharama za uendeshaji,” amesema Makolobela.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea na mpango wa kufanya tafiti zaidi katika maeneo ya madini ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wenye tija.


“Wito wangu kwa taasisi za kifedha ni kuangalia upya namna ya kuwakopesha wachimbaji wadogo, kwa kuwa wana bidhaa halisi, masoko yapo, na taarifa zao za kifedha zinajulikana. Wana uwezo wa kurejesha mikopo,” amesisitiza Makolobela.

Amebainisha kuwa kwa sasa Mkoa wa Simiyu una vituo vitano vya ununuzi wa madini na soko kuu moja lililopo Bariadi Mjini, ambako shughuli kubwa za biashara ya madini hufanyika.

Makolobela pia amewapongeza wachimbaji kwa kuendelea kushiriki katika shughuli za kijamii kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), akitaja mfano wa vikundi vya TAWOMA na EMJ vilivyotoa zaidi ya madawati 90 kwa Shule ya Majengo kama sehemu ya kurudisha kwa jamii.


 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI