Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa madini kupitia programu jumuishi ya Mining for Better Tomorrow (MBT), inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake kunufaika moja kwa moja na rasilimali za taifa.
Dhamira hiyo imesisitizwa leo, Novemba 27, 2025, na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, wakati akizungumza na mamia ya wachimbaji wadogo vijana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lemshuku, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Akizungumza kwa msisitizo, Waziri Mavunde amesema anataka kuona uchumi wa madini nchini ukimilikiwa na Watanzania wenyewe, na kwamba Tanzania inakuwa kitovu cha biashara ya madini barani Afrika endapo yatawekewa miundombinu sahihi na uwezeshaji kwa wananchi.
“Natamani kuona Mirerani, Arusha, Geita, Chunya, Mara,Kahama na maeneo mengine nchini yanakuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na metali Afrika. Nataka kuona Dubai ikihamia Simanjiro,” amesema Mavunde huku akishangiliwa na wachimbaji vijana.
Zaidi ya vikundi 21 vyenye jumla ya wanachama 423 vimekabidhiwa leseni katika ziara hiyo, ambayo vikundi 7 vyenye jumla ya wachimbaji 127 vimapewa leseni za uchimbaji mdogo wa tanzanite na vikundi 14 vyenye wanachama 296 vimepewa leseni za kufanya biashara ya tanzanite, hatua iliyorasimisha vikundi hivyo kwenye mnyororo wa thamani wa tanzanite.
Katika ziara hiyo, Waziri Mavunde ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo kipya cha ununuzi wa madini cha Lemshuku, mradi unaotarajiwa kuwa mkombozi kwa wachimbaji wadogo kupitia mfumo rasmi wa masoko. Ujenzi huo umefikia asilimia 88, na Waziri amemwelekeza Afisa Madini Mkazi wa Mirerani kuongeza kasi ya ujenzi ili kituo kikamilike na kuanza kufanya kazi mapema iwezekanavyo.
Katika mkutano huo, Waziri ametumia muda kuzungumza moja kwa moja na wachimbaji pamoja wamiliki wa leseni za madini ya vito, akisikiliza changamoto zinazowakabili ambapo ameahidi kuzifanyia kazi mara moja changamoto za maji, miundombinu, umeme, usalama, vibali na huduma za kijamii kwani Serikali ni moja na huduma hizo ni kichocheo muhimu katika maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji.
Akikumbusha ahadi alizotoa katika ziara yake ya awali, Waziri Mavunde amesema ujenzi wa kituo cha afya cha Lemshuku nao unaendelea na ujenzi, na juhudi za kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wanapata huduma ya maji safi zinaendelea. Huduma hizo zinatarajiwa kuboresha ustawi wa wachimbaji na jamii inayowazunguka.
Kwa kuhitimisha, Waziri Mavunde amewata vijana na watanzania kwa ujumla kulinda amani ya nchi ili kufanya maendeleo na kutimiza majukumu yao maana hawana Tanzania nyingine.














0 Comments