Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umetangaza kuungana na Watanzania wote kuomboleza vifo vya wananchi, wakiwemo waandishi wa habari wenzao, vilivyotokea siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kupitia taarifa yake ya Novemba 8, 2025, UTPC imetoa pole za dhati kwa wananchi waliopoteza mali na familia zilizopoteza wapendwa wao, huku ikiwaombea uponyaji wa haraka wale waliojeruhiwa kimwili, kisaikolojia na kiroho.
Umoja huo umetoa wito kwa serikali, sekta binafsi, viongozi wa dini, mashirika ya kiraia, sekta ya habari na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kujenga maridhiano na mustakabali wa pamoja kwa manufaa ya taifa, ambalo limekuwa kisiwa cha amani na mfano kwa mataifa mengine.
UTPC imetambua athari za kisaikolojia zilizosababishwa na matukio hayo, ikiwemo kwa wale waliotazama picha mnato na picha mjongeo za vurugu hizo. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, umoja huo umepanga kutoa msaada wa kisaikolojia na kijamii (Psychosocial Support) kwa waandishi wa habari na wanajamii watakaohitaji msaada huo.
Vilevile, UTPC imeziomba taasisi za serikali na binafsi kushirikiana kutoa msaada huo kwa mtu mmoja mmoja, vikundi na familia zilizoathirika, hatua ambayo itachochea uponyaji wa haraka.
Aidha, imetoa wito kwa makundi yote kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama wa watu na mali zao, ikisisitiza kuwa amani ni zao la haki, na utu ni kiini cha amani.








0 Comments