Header Ads Widget

UJENZI WA VYUO 65 VETA KUKAMILIKA 2026

 

Na Lilian Kasenene, MorogoroMatukio DaimaApp 

SERIKALI imeendelea kusogeza huduma za mafunzo stadi hasa kwa vijana kwa kuweka nguvu katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kwa vyuo vya Mamlaka ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).


Kwa sasa vyuo 80 vinatoa huduma ya mafunzo na 65 vikiwa bado katika hatua ya ujenzi kwa Halmashauri zote nchini.


Hayo yamebainishwa na Mjumbe wa Bodi ya VETA Abdulhamad Masai wakati wa hafla ya mahafali ya 28 ya Chuo cha VETA Mikumi.


Akisisitiza alisema mpango wa serikali ni kujenga vyuo 145 kote nchini, matarajio ni ujenzi wake kukamilika mwaka ujao wa 2026, ili kuwezesha Watanzania kupata mafunzo ya ustadi katika vyuo hivyo.


Alisema hatua hiyo katika eneo la utoaji elimu na mafunzo ni sehemu ya mkakati wa serikali ya kutimiza dhima ya kuzalisha mafundi katika nyanja mbalimbali, akihimiza jamii kuona fursa zilizopo VETA pamoja na kutumia wataalamu wanaozalishwa na vyuo hivyo 


Aidha alihimiza wahitimu hao, kuhakikisha wanaifikia fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kupitia Halmashauri zake kwa kuunganisha nguvu za pamoja kwa kuunzisha kampuni au biashara kisha kuzisajili ili kuwawezesha kupata mikopo hiyo itakayowasaidia kuendeleza ujuzi wao na kufikia malengo tarajiwa.


"Sehemu ya kwanza naweza kuwaambia nyie wahitimu katumieni hii fursa ya mikopo ya Halmashauri, huwezi kuwa fundi umeme kama huna leseni, kajisajilini mpate leseni na mkajiunge kwa pamoja hata watu watatu muanzishe kampuni au biashara itakayowasaidia kupata mikopo ya kuwaendeleza kimaisha" Amesema Masai


Awali Mkuu wa Chuo cha VETA Mikumi Marynurce Kazosi amesema pamoja na chuo hicho kuwa kikongwe wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa na maeneo ya kujifunzia kwa vitendo hali ambayo imekuwa ikiwawia vigumu kutoa mafunzo kulingana na mahitaji huku miundombinu na mashine za kufundishia zikiwa haziendani na teknolojia ya sasa.


"Mgeni rasmi, umejionea eneo letu la magari na mechanics bado tunachangamoto hizo, tunaomba hilo pia ulibebe ili chuo chetu tuweze kutengenezewa miundombinu kuhakikisha vijana wetu wanatoka na ujuzi ambao ni mahiri" Amesema Marynurce 


Kwa upande wake Mariam Temekele Mhitimu wa fani ya ufundi magari VETA Mikumi, amesema wazo lake kujifunza fani hiyo amelipata mwaka 2022 baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari 2020 na kukaa sana mtaani, ambapo aliamua kuwashirikisha wazazi wake ambao waliridhia na kuamua kujiunga na chuo hicho, imani yake ni wasichana kujitokeza kwa wingi kusomea fani hiyo na kuacha kuamini ni ngumu na ipo kwa ajili ya vijana wa kiume pekee.


"Sisi sote tuna usawa ni wanaume na wanawake ni 50 kwa 50, watu wengi wanasikiliza maneno kwamba fani fulani fulani ni ngumu kumbe sio kweli, hata mimi niliambiwa fani ya ufundi magari ni ngumu lakini sasa naona hakuna ukweli wowote, kikubwa ni uaminifu na kujiamini,"alisema Mariam


Alisema jambo la muhimu ni wasichana kuondoa dhana ya kwamba kazi hiyo inakufanya uonekane mchafu wakati wote, akisisitiza kwa anayezingatia usafi hawezi kuonekana mchafu, bali akiamua kuuishi uchafu au hali ya uchafu ataonekana hivyo.


Naye Bahati Mussa mhitimu wa fani ya uchomeleaji na uundaji wa vyuma, anawasihi pia vijana wa kike kutoona ugumu kwa fani hiyo, kwa kuwa maisha ya sasa hayana fani ya wanaume au wanawake, akisisitiza kuwa kazi yoyote wanaweza kuifanya kwa ustadi, uaminifu na umahiri wakaweza kufikia lengo.


Katika mahafali 28 katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mikumi jumla ya wahitimu 271 wametunukiwa vyeti vya fani mbalimbali ambapo ngazi ya pili wapo wahitimu 172 na ngazi ya tatu wapo 99.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI