Na chausiku said, Matukio Daima Mwanza.
CHAMA cha Wateknolojia Dawa Tanzania (TAPHATA), kwa kushirikiana na vyama vingine vya kitabibu, limefanya mkutano wake wa 26 Jijini Mwanza, ambapo wataalamu wa afya walikusanyika kujadili namna ya kuboresha huduma za kitabibu na kuhakikisha upatikanaji wa dawa salama kwa wananchi.
Rais wa TAPHATA, Thabit Milandu, alisema kuwa kongamano hili ni sehemu muhimu ya kubadilishana uzoefu, kujiimarisha katika teknolojia ya dawa, na kujenga ushirikiano miongoni mwa wataalamu wa sekta ya afya huku akieleza lengo kuu la mkutano huu ni kuharakisha maendeleo ya sekta ya afya nchini, kwa kuhakikisha kwamba teknolojia ya dawa inachangia katika kuhakikisha huduma za matibabu ni bora, salama, na zinapatikana kwa urahisi.
"Tunahitaji kubadilishana maarifa na uzoefu ili tuweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya afya. Huu ni wakati wa kuhakikisha dawa zinapatikana kwa bei nafuu, zinakuwa salama, na kuwa na mifumo bora ya usambazaji," alisema Milandu.
Kongamano hilo pia likilenga kutambua na kutoa tuzo kwa wataalamu wa teknolojia ya dawa ambao wamefanikiwa katika kuboresha huduma za afya nchini. Zaidi ya washiriki 1,000 walihudhuria mkutano huu, ambao ulianza tarehe 26 Novemba na unatarajiwa kumalizika Novemba 28. Kauli mbiu ya mwaka huu ilikua: "Kuwezesha Wateknolojia Dawa, Kubuni na Kuendeleza Mustakabali wa Teknolojia ya Dawa Nchini Tanzania - Dawa Salama, Taifa Salama."
Rais Milandu alisisitiza kuwa kongamano hili linatoa nafasi muhimu ya kutafakari na kujadili masuala yanayohusu upatikanaji wa dawa salama, huku pia kuhakikisha kuwa hospitali za serikali zinapata dawa muhimu kwa wakati na kwa kiasi kinachohitajika.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwahamasisha wataalamu wa dawa kutovunjika moyo kutokana na changamoto ya ukosefu wa ajira, akiongeza kuwa fani ya teknolojia ya dawa ina fursa nyingi za kujiajiri. Alisema, "Serikali inatoa mikopo kwa wateknolojia dawa ili waweze kuanzisha na kuendeleza biashara zao, hivyo hakuna sababu ya kukata tamaa."
Mtanda pia alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili ya kazi na kuwataka wataalamu wa sekta ya afya kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii. Alisema serikali ina mpango wa kuongeza ajira zaidi ya 10,000 katika sekta ya afya, hivyo aliwahimiza vijana kujiandikisha na kuomba nafasi hizo.
Msajili wa Baraza la Famasi, Boniface Magige, alisema kuwa kongamano hilo linatoa fursa ya kutathmini hali ya maadili ya wataalamu wa dawa na kuhamasisha usimamizi mzuri wa rasilimali za dawa. Alisema, "Tunaendelea kupambana na wale wanaojinufaisha kwa kuuza dawa zinazotolewa na serikali kwa bei ya juu, jambo ambalo linavuruga mfumo mzima wa upatikanaji wa dawa."
Mteknolojia Dawa Mwandamizi, Janeth Kipanda, alieleza juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuhakikisha dawa zisizo salama hazingii sokoni. Alisema, "Tunatekeleza mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa dawa zote zinazozunguka sokoni zinakaguliwa na kuthibitishwa kuwa salama kabla ya kupatikana kwa watumiaji."
Mfamasia kutoka Bohari ya Madawa (MSD), Mussa Sayyida, alisema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya dawa muhimu zinazotumika nchini zinazalishwa ndani ya nchi, na serikali imeweka juhudi kubwa katika kuboresha uwezo wa viwanda vya dawa vya ndani. "Serikali inaendelea kuwekeza katika viwanda vya dawa kama vile Idofe Pharmaceutical, Keko Pharmaceutical, na Arusha Pharmaceutical, ili kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana kwa bei nafuu na kwa wingi."
Mwisho.











0 Comments