Na Mwandishi Wetu, Iringa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) leo umepokea magari mawili mapya aina ya Toyota Land Cruiser yenye thamani ya Sh323 milioni kutoka Southern Tanzania Elephant Program (STEP), katika hafla iliyofanyika asubuhi katika ofisi za STEP, Wilolesi mkoani Iringa mapema leo November 24,2025
Makabidhiano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Mandhari ya Udzungwa (ULS) unaolenga kuongeza nguvu ya ulinzi, doria na ufuatiliaji katika Hifadhi Asilia za Udzungwa na Kilombero—maeneo yenye bioanuwai adimu na vyanzo muhimu vya maji kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Prof. Dos Santos Silayo, Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali TFS na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Dk. Zainabu Bungwa, alisema msaada huo utaboresha uwezo wa watumishi kufika maeneo ya mbali kwa haraka na kuimarisha doria dhidi ya uvamizi na ukataji miti holela.
“TFS inathamini ushirikiano wa STEP na wadau wengine. Tunahakikisha magari haya yanatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kwa utunzaji unaostahili,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa STEP, Frank Lihwa, alisema msaada wa magari unafuatia juhudi za kuimarisha uhifadhi zilizoanza mwaka 2016/17, ikiwemo mafunzo kwa Kamati za Maliasili za Vijiji (VNRCs), Askari wa Wanyamapori Vijijini (VGS), walinzi wa misitu, pamoja na utoaji wa vifaa vya drones, kamera na mawasiliano.
“Magari haya yataongeza ufanisi wa doria na kutupa uwezo wa kufuatilia vitisho kwa wakati,” alisema Lihwa.
Akiwasilisha hotuba ya Prof. Silayo, Dk. Bungwa alieleza kuwa pamoja na umuhimu wa misitu ya Udzungwa kama kitovu cha bioanuwai na chanzo cha maji, bado inakabiliwa na changamoto za uvamizi, ukataji holela na uwindaji haramu.
ULS unatekelezwa kwa pamoja na STEP, MACCO, TFS na TANAPA, kwa ufadhili wa Hempel Foundation na Aage V. Jensen Charity Foundation, ikiwa ni mpango wa miaka 20 unaolenga kuimarisha ulinzi wa misitu, ushiriki wa jamii na uhifadhi wa bioanuwai.
TFS imewataka wadau kuongeza nguvu katika maeneo mengine yenye vitisho vya uharibifu ikiwemo misitu ya Rungwe, Kalambo, Njombe na Mbeya.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kuhamasisha uhifadhi,” imesema hotuba hiyo.

.jpg)











0 Comments