Morogoro
Sekta ya madini nchini inatarajia kupata sura mpya baada ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) kusaini makubaliano ya kuanza tafiti za madini ya kimkakati zitakazowezesha uchakataji, uongezaji thamani na uzalishaji kufanyika ndani ya Tanzania.
Makubaliano hayo, yaliyotiwa saini mjini Morogoro, yanatajwa kuwa hatua ya kihistoria inayolenga kuondoa utegemezi wa kuuza madini ghafi nje ya nchi na badala yake kuyaendeleza kwa teknolojia za ndani.
Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, CPA Dkt. Venance Mwasse, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya serikali kuhakikisha sekta ya madini inachangia moja kwa moja katika ajira, kodi na ukuaji wa viwanda.
“Kwa muda mrefu tumeuza madini ghafi. Sasa tunataka kila thamani ibaki hapa nyumbani. Tafiti hizi zitatoa ajira, kuongeza ujuzi na mapato ya Serikali,” alisema Dkt. Mwasse.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TIRDO, Prof. Mkumbukwa Madundo, alisema ushirikiano huo unaunganisha nguvu za kisayansi na teknolojia za ndani ili kuhakikisha Tanzania inakuwa sehemu ya nchi zinazotumia teknolojia safi kuchakata madini.
“Tunakwenda kuchakata madini kwa kutumia ubunifu na mitambo ya kisasa, tukiweka mbele ajenda ya nishati safi na ulinzi wa mazingira,” alisema Prof. Madundo.
Madini kama lithium, graphite na rare earths, yanayohitajika katika utengenezaji wa betri, magari ya umeme na vifaa vya mawasiliano, yanatajwa kuwa miongoni mwa madini yatakayofanyiwa utafiti huo wa miaka miwili.
Utafiti huu unakwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, inayolenga kujenga uchumi wa viwanda unaotumia rasilimali za ndani na kulinda mazingira.










0 Comments