Header Ads Widget

IDADI NDOGO YA WABUNGE PINZANI BUNGENI SIO UDHAIFU BALI NI FURSA


Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media

MBUNGE wa Jimbo la Segerea, Agnesta Kaiza, amesema kuwa idadi ndogo ya wabunge kutoka upande wa upinzani haipaswi kuonekana kama udhaifu, bali kama fursa ya kuonesha ubora na uthubutu katika hoja zenye tija kwa taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari bungeni jijini Dodoma, Mhe. Kaiza amekumbuka kipindi alipokuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akieleza namna walivyoweza kufanya kazi kwa ufanisi licha ya kuwa wachache ndani ya Bunge.

“Kwanza nilikuwa ni mbunge wa viti maalum kupitia CHADEMA tulikuwa wachache, tulijulikana kama kundi la wachache bungeni, lakini nyinyi waandishi ni mashahidi  tulifanya kazi nzuri sana pamoja na kwamba hatukuwa na kambi rasmi ya upinzani, hoja zetu nyingi zilisikika,” amesema Mhe. Kaiza.

Akiendelea kueleza mtazamo wake kuhusu nafasi ya wachache katika mageuzi ya Bunge, Mhe. Kaiza amesema kuwa mabadiliko ya kweli hayahitaji wingi wa watu bali uthabiti wa hoja na dhamira ya dhati.

“Naamini katika masuala ya mabadiliko au kusimamia jambo, si lazima uwe na wingi mkubwa wakati mwingine wingi siyo majibu ya ubora wa mambo kufanyika,” ameongeza.

Mbunge huyo amehitimisha kwa kueleza imani yake kuwa pamoja na uchache wao, wataweza kuleta tofauti kubwa yenye manufaa kwa Watanzania ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Naamini katika uchache wetu, tunakwenda kuleta tofauti kubwa sana yenye tija ndani ya Bunge,” amesema kwa matumaini.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI