.
Na,Jusline Marco :Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Makalla amekishukuru Chama cha Waongoza Watalii nchini Tanzania (TATO) ushirikiano wao na Kamati hiyo katika kipindi cha matukio ya Uvunjifu wa amani Oktoba 29, 2025 pamoja na wanavyoendelea na jitihada zao za kuutangaza utalii wa Tanzania Kimataifa.
CPA Makalla ametoa pongezi hizo Novemba 27 wakati ameongoza Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Arusha, wajumbe wa Kikao hicho wakijiridhisha kuwa shughuli za Utalii zinaendelea vizuri huku idadi kubwa ya Watalii ikishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Vivutio Mkoani hapa.
"Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama niendelee kuhamasisha watalii kuja Mkoani Arusha, niwahakikishie hali ya usalama ni shwari na wale wanaopanga safari zao za kwenda Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro, Serengeti na Tarangire, karibuni Jiji la Arusha." Amesema Mhe. Makalla.
Aidha amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuutangaza Utalii wa Tanzania, huku akisema Kamati ya Ulinzi na usalama itaendelea kulinda Vivutio vya Utalii vilivyopo Mkoani Arusha pamoja na kuhakikisha usalama wa watalii kwa muda wote.
Ameongeza kwa kuwataka Wajumbe wa Kamati hiyo wakiwemo Wakuu wa Wilaya sita za Mkoa wa Arusha, kuendelea kuimarisha usalama katika maeneo yao, kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo pamoja na kusimamia maandalizi ya msimu mpya wa Masomo na Kilimo unaotarajiwa kuanza mapema Januari mwaka 2026.








0 Comments