NA FARIDA MANGUBE MATUKIO DAIMA APP, MOROGORO
CHUO Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Afya kimetoa mafunzo ya uongozi kwa Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Halmashauri nchini na vituo vya afya ikiwa ni jitihada za kuongeza ufanisi katika usimamizi wa huduma za afya na kuhakikisha uwekezaji mkubwa wa serikali kwenye sekta hiyo unaleta tija kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo ya siku tano yaliyofanyika mkoani Morogoro, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Tumain Nagu, aliipongeza Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutambua umuhimu wa kuwajengea uwezo viongozi wa afya.
Alisisitiza kuwa huduma bora katika vituo vya afya zinategemea uongozi thabiti, matumizi sahihi ya takwimu na uwajibikaji.
Prof. Nagu alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwekeza kikamilifu katika miundombinu ya sekta hiyo, ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya zaidi ya 700 na uwekezaji wa zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kwa ajili ya kuboresha huduma kuanzia ngazi ya msingi.
Mafunzo hayo ambayo pia yamewezeshwa na wadau kama Global Fund, yamelenga kuwaongezea washiriki uwezo wa uongozi, upangaji mikakati, pamoja na usimamizi wa rasilimali ili kuboresha utoaji wa huduma katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Henry Mollel, alisema chuo kimeamua kushirikiana na Serikali ili kuzalisha viongozi wenye weledi watakaoweza kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu katika vituo vya afya.
“Mafunzo haya yanalenga kuongeza tija na kuhakikisha uwekezaji wa serikali unaleta matokeo yanayoonekana,” alisema.
Naye Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Gabriel Komba, alisema washiriki wamepatiwa uelewa mpana kuhusu uongozi bora na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi yenye makusudi na yenye kuleta matokeo.
Washiriki wa mafunzo hayo walisema yamewasaidia kupata mbinu mpya za kutatua changamoto katika vituo vya afya na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma. “Tumeshirikishana uzoefu na tumejifunza mbinu ambazo zitaongeza ubora wa kuhudumia wananchi,” walisema.
Mwisho.








0 Comments