Header Ads Widget

MKE WA BESYIGE AMSHUTUMU RAIS MUSEVENI KUMUANDAA MTOTO WAKE KUMRITHI

 

Bi. Winnie Byanyima, mke wa kiongozi wa upinzani wa Uganda aliyekamatwa Dkt. Kizza Besigye, amemshutumu rais wa nchi hiyo mwenye umri wa miaka 81, Yoweri Museveni, kwa kumtayarisha mwanawe kumrithi.

Pia alifichua kwamba mumewe, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini, alikamatwa kwa kusema kile alichokielezea kama urithi wa kisiasa uliopangwa.

"Tunamwona akitupeleka katika mwelekeo hatari wa kumweka mwanawe, [Jenerali Muhoozi Kainerugaba] ambaye tayari amemteua kama mkuu wa jeshi, kuwa rais wetu ajaye. Na ndiyo maana naamini Dkt. Kizza Besigye yuko gerezani, kwa sababu amesema vikali dhidi ya mradi huo. Anaona ni hatari, na nakubaliana naye," aliambia BBC.

Matamshi yake yanakuja mwaka mmoja baada ya Dkt. Besigye, kiongozi maarufu wa upinzani, kukamatwa kwa utata katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Akizungumzia hali yake, Bi. Byanyima alisema kwamba Dkt. Besigye ametengwa peke yake gerezani. "Haruhusiwi kuzungumza na wafungwa wengine; hawezi kuabudu pamoja na wafungwa wengine; hawezi kucheza mchezo wa mpira wa miguu na wengine; haruhusiwi kuzungumza [au] hata kumsalimia mfungwa mwingine. Kwa hivyo amekuwa kizuizini kwa mwaka mmoja sasa."

Bi. Byanyima alisisitiza kutokuwa na hatia kwa mumewe na kukosoa mfumo wa haki wa nchi, akisema "umekamatwa na Rais Museveni."

Aliongeza kuwa hana matumaini makubwa kwamba haki itapatikana.

Dkt. Besigye alikamatwa awali mnamo Novemba mwaka jana jijini Nairobi pamoja na msaidizi wake, Obeid Lutale.

Siku chache baadaye, walijitokeza tena mbele ya mahakama ya kijeshi huko Kampala, ambapo walishtakiwa kwa uhaini na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Hata hivyo, kesi hiyo baadaye ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia baada ya mahakama kuu ya nchi hiyo kuzuia kesi ya raia katika mahakama za kijeshi.

Wawili hao, pamoja na afisa wa kijeshi, sasa wanakabiliwa na mashtaka mapya ya uhaini, kosa linaloadhibiwa kwa kifo au kifungo cha maisha. Hawajakiri shutuma zinazowakabili.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI