Ronaldo ambaye alizaliwa katika kisiwa cha Madeira alikuwa tayari ameonyesha kuwa anapenda kusoma, na pia kuvutiwa na masuala ya sayansi
Nyota wa soka Cristiano Ronaldo anatarajiwa kutembelea Ikulu ya White House Jumanne, siku ileile Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, atakapokuwa hapo.
Ingawa White House haikuthibitisha kama Ronaldo ni sehemu ya msafara wa mwanamfalme, nafasi yake kama uso wa mageuzi ya soka nchini Saudi imemfanya kuwa mchezaji muhimu katika juhudi za taifa hilo kupanua uchumi kupitia michezo na utalii.
Ronaldo hajarejea Marekani tangu 2016. Katika kipindi hicho, alikabiliwa na madai ya ubakaji kutoka kwa Kathryn Mayorga, madai aliyoyakanusha akisema: "Ubakaji ni uhalifu wa kuchukiza ambao unaenda kinyume na kila kitu nilicho na kuamini.’’
Mwaka 2019, waendesha mashtaka wa Marekani walisema hakuna mashtaka yatakayomkabili kwa kuwa madai hayo hayakuthibitishwa.
Mwaka 2023, Ronaldo alijiunga na timu ya Al Nassr na kuwa uso wa ligi ya Saudi, akilipwa takribani dola milioni 200 kwa mwaka.
Juni mwaka huu alisaini mkataba mpya wa miaka miwili unaokadiriwa kufikia dola milioni 400, na Bloomberg ilimwita mchezaji wa kwanza wa soka kuwa bilionea, akiwa na utajiri wa dola bilioni 1.4.
Kwa mujibu wa Sanam Vakil wa Chatham House, Saudi Arabia imewekeza “katika matukio na nyota wakubwa wa soka” ili kuutambulisha ufalme duniani kupitia michezo na utalii.
Ronaldo, anayemwita mwanamfalme “bosi wetu,” hivi karibuni alihudhuria hafla ya Wizara ya Utalii Riyadh na kutangaza matumaini yake kuwa Kombe la Dunia 2034 litafanyika Saudi Arabia.
Kuhusu kukutana na Rais Trump, Vakil anasema Trump “anapenda vitu vinavyong’aa, na Ronaldo ni kitu kinachong’aa.”
Ronaldo naye amemtaja Trump kama mtu anayetamani kukutana naye kwa ajili ya juhudi za “amani ya dunia,” na alimkabidhi jezi ya Ureno iliyosainiwa na Ronaldo yenye ujumbe: “Kwa Rais Donald J. Trump, Playing for Peace.”
Trump amekwishakutana na mwanamfalme katika Ofisi ya Oval, na wote wawili wanatarajiwa kuhudhuria dhifa ya kifahari katika East Room ambapo Ronaldo pia anatarajiwa kuwepo.
White House haijatoa orodha rasmi ya wageni, lakini inatarajiwa kujumuisha wakuu wa makampuni makubwa ya Marekani yenye ushirikiano wa kibiashara na Saudi Arabia.






0 Comments