Na Matukio Daima Media
Kwa zaidi ya muongo mmoja, jina la Dk. Mwigulu Lameck Nchemba limeendelea
kung’aa katika anga la siasa na uchumi wa Tanzania. Ni miongoni mwa viongozi
wachache wanaojulikana kwa umakini, uzalendo na uelewa mpana wa masuala ya
fedha za umma.
Dk. Nchemba, ambaye alizaliwa tarehe
7 Januari 1975 katika Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida, ni
mwanachama wa muda mrefu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na amekuwa Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi tangu mwaka 2010.
Safari yake ya elimu ni kielelezo
cha bidii na kujituma akiwa kijana kutoka kijijini, Mwigulu alikua na ndoto ya
kuwa mchumi mashuhuri alisomea Shahada
ya Kwanza ya Uchumi katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kisha kuendeleza masomo ya Uzamili (MA in Economics) na
hatimaye Uzamivu (PhD in Economics)
katika chuo hicho hicho.
Utaalamu wake katika uchumi ulimpa
msingi imara wa kuingia katika utumishi wa umma, ambapo alihudumu awali kama
mchambuzi wa sera za uchumi katika Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) na baadaye katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwaka 2010, Mwigulu alichaguliwa kwa
mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Jimbo la
Iramba Magharibi, jambo lililomfungulia ukurasa mpya wa maisha yake ya
kisiasa. Umahiri wake ulimfanya kuaminiwa na viongozi wakuu wa serikali, na
tangu wakati huo ameshika nafasi kadhaa muhimu:
- 2012–2015:
Naibu Waziri wa Fedha
- 2015–2016:
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi
- 2016–2018:
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi
- 2020–2021: Waziri wa Katiba na Sheria
- 2021–2025: Waziri wa Fedha na Mipango
- 2025–Sasa: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Machi 31, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Dk. Nchemba kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, nafasi aliyoitumia kuimarisha nidhamu ya matumizi ya fedha, kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuhimiza matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha za umma.
Akiwa Waziri wa Fedha, alisimamia utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) na kufanikisha ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na taasisi za kimataifa kama IMF, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Tarehe 13 Novemba 2025, Rais Samia Suluhu Hassan amemteua rasmi Dk. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ya juu kabisa serikalini baada ya Makamu wa Rais.
Uteuzi huo umepokelewa kwa pongezi nyingi kutoka ndani na nje ya chama chake, huku wengi wakimpongeza kwa uadilifu, weledi na uzoefu mkubwa katika masuala ya kiuchumi na uongozi.
Dk. Nchemba amekuwa akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na nidhamu ya fedha katika taasisi za umma. Kauli yake maarufu ni:
“Rasilimali tulizo nazo ni chache, tunapaswa kuzitumia kwa tija ili kizazi kijacho kinufaike.”
Anaamini kuwa maendeleo ya kweli yanatokana na mipango sahihi, uwazi wa kifedha, na matumizi bora ya kodi za wananchi.
Kutoka mchumi wa BoT hadi Waziri Mkuu, Dk. Nchemba amejidhihirisha kuwa kiongozi wa kizazi kipya mwenye dira, uthubutu na maono ya kiuchumi.









0 Comments