Header Ads Widget

MC PILIPILI AFARIKI DUNIA BAADA YA KUSHAMBULIWA, POLISI DODOMA WACHUNGUZA CHANZO

 

Na  Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma.

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma limethibitisha kifo cha msanii maarufu wa vichekesho Emmanuel Mathias Matebe, maarufu kama MC Pilipili, kilichotokea Novemba 16, 2025 katika Kituo cha Afya Ilazo, jijini Dodoma, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Novemba 19, 2025, Kamishna Msaidizi wa Polisi William Mwamafupa alisema kuwa MC Pilipili alifikishwa kituoni hapo akiwa katika hali mbaya na alifariki dunia majira ya saa 9:00 alasiri.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, kabla ya kifo chake, majira ya saa 8:00 mchana, msaidizi wake Hassan Ismail alipigiwa simu na mtu asiyefahamika na kuitwa mahali fulani kwa mazungumzo. 

Baada ya muda, walitokea watu watatu ambao hawakufahamika wakimtumia MC Pilipili wakiwa ndani ya gari dogo jeupe na kumkabidhi kwa msaidizi wake kisha kuondoka kwa haraka.

Wataalamu wa afya kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamebaini kuwa marehemu alionyesha dalili za kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili, hali iliyosababisha majeraha makubwa na hatimaye kifo.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa kina unaendelea ili kuwabaini wahusika wa tukio hilo na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.

Kifo cha MC Pilipili kimetikisa tasnia ya sanaa na burudani nchini, ambapo wasanii na wafuasi wake wameendelea kumiminika mitandaoni kutoa salamu za rambirambi na kushangazwa na mazingira ya kifo chake.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI