Header Ads Widget

MADEREVA KILIMANJARO WACHANGAMKIA FURSA ZA USAFIRI WA MTANDAONI (BOLT)

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA

Kampuni ya usafiri wa mtandaoni, Bolt Tanzania, imezindua rasmi huduma zake katika mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro, hatua inayoonekana kama mafanikio makubwa katika juhudi za kuleta suluhisho la usafiri wa kisasa, wa kuaminika na nafuu.

Ujio wa Bolt Moshi unatarajiwa kubadilisha namna ambavyo wakazi, wafanyabiashara wadogo na wasafiri wa kila siku wanavyosafiri kutoka eneo moja kwenda jingine katika mji huu maarufu kwa shughuli za biashara na utalii.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Moshi, Mtaalam wa Huduma za Usafirishaji wa Bolt Tanzania, Kenji Michael, alisema “Mji wa Moshi ni lango kuu la watalii wanaokuja kuanza safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro, ni mji wenye shughuli nyingi za kiuchumi, kuingia kwetu katika eneo hili ni sehemu ya dira ya Bolt ya kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Moshi.”



Aliongeza kuwa huduma hiyo itatoa ajira zaidi kwa vijana kupitia usajili wa madereva washirika, hatua itakayoongeza mzunguko wa wateja na kuimarisha biashara za eneo hilo.

Kenji alisema kabla ya ujio wa Bolt, baadhi ya wakazi walilazimika kupiga simu ili kupata bajaji, na maeneo mengine hayakufikiwa kabisa, kupitia huduma ya Bolt LATRA D4, abiria sasa wanaweza kufikiwa popote ndani ya Manispaa ya Moshi.


"Mwitikio wa madereva wa bajaji na abiria kujiunga na huduma yetu umekuwa mkubwa sana, lengo letu ni kuwawezesha madereva na kuhamasisha abiria kuchangia kukuza uchumi wa maeneo yao,” alisisitiza.


Hata hivyo, alitaja changamoto ya baadhi ya madereva kutumia simu za zamani zinazochelewesha upakiaji wa ramani, jambo ambalo linaathiri ufanisi wa huduma, pamoja na changamoto hiyo, alisema ushirikiano kati ya Bolt na watoa huduma wa bajaji umeendelea kuwa mzuri na umechochea ukuaji wa biashara.


“Zamani madereva walikuwa wanafanya kazi kwa masaa machache, lakini sasa wanafanya kazi saa 24, jambo ambalo limepanua wigo wa kipato chao,” alisema.

Mmoja wa madereva wa bajaji, Selemani, alisema amejiunga na huduma ya Bolt baada ya kupata ushuhuda kutoka kwa madereva wengine waliokuwa tayari wanatumia jukwaa hilo.

“Tulikuwa tunakaa vijiweni muda mrefu bila kupata kazi, kujiunga na Bolt kumetusaidia sana kupata wateja kwa wakati tofauti na wale ambao hawajajiunga,” alisema Selemani.

Naye Anjela Mwagala alisema kuwa madereva wa bajaji na bodaboda wana nafasi ya kujiandikisha na kutumia mtandao wa Bolt ili kuongeza wigo wa kupata wateja.

Kwa upande wake, Hanser Alfred aliwahamasisha wakazi wa Moshi kujiunga na kutumia huduma hizo hasa katika misimu ya sikukuu, ili wageni kutoka mikoa mingine wapate huduma kwa urahisi na usalama.


MWISHO.

KARIBU KUTANGAZA NA MATUKIO DAIMA MEDIA KUPITIA INSTAGRAM, TIKTOK, FACEBOOK, X, APP NA CHANEL YA MATUKIO DAIMA TV PIGA SIMU 0754026299


Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI