Header Ads Widget

KIZUNGUMKUTI MCHAKATO WA UMEYA MANISPAA YA IRINGA

Mstahiki meya mstaafu na mgombea tena nafasi hiyo Ibrahim Ngwada 

Na Matukio Daima Media, Iringa

Mvutano wa chini kwa chini kuhusu nafasi ya Umeya wa Manispaa ya Iringa umeibuka upya baada ya kuenea kwa fununu zinazodai kuwepo kwa mvurugano katika hatua za awali za mchujo wa wagombea.

Tetesi  hizo ambazo zimekuwa zikizungumzwa na baadhi ya wadau wa siasa za Iringa Mjini zinadai kwamba huenda kulikuwa na harakati za chini kwa chini zinazotajwa kuhusisha baadhi ya madiwani kuhamasishwa kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwa malengo yanayodaiwa kumpa mgombea fulani mazingira rafiki ya kupenya katika mchujo.


Hata hivyo, madai hayo yamekanushwa vikali na mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Iringa Mjini, ambaye amesisitiza kuwa taratibu za chama zimefuatwa kikamilifu na kwamba hakuna mipango yoyote ya kupendelea mgombea yoyote.

Kwa mujibu wa taarifa za baadhi ya wadau wanaofuatilia zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu, zinaonesha awali waliowasilisha fomu walikuwa watatu tu.

Hata hivyo, baada ya muda wa kurejesha fomu kukamilika, taarifa zisizo rasmi zilidai kuwa idadi ya wagombea iliongezeka na kufikia sita jambo lililoibua maswali kutoka kwa baadhi ya watu wanaofuatilia uchaguzi huo.

“Novemba 20 ndiyo ilikuwa siku ya kuchukua fomu na watatu tu walichukua. Kesho yake, Novemba 21, wote watatu walirudisha fomu. 

Lakini jana taarifa zilizosambaa zilidai kuwa wagombea sasa ni sita,” kilisema chanzo kimoja kutoka miongoni mwa wadau wa uchaguzi huo, kikisisitiza kuwa hali hiyo imeacha maswali bila majibu.

Wakili Chaula Mgombea umeya 

Wagombea wa awali waliorudisha fomu kwa mujibu wa taarifa hizo ni pamoja na aliyekuwa Meya wa Manispaa hiyo awamu iliyopita, Ibrahim Ngwada (Diwani wa Mshindo), Jackson Chaula (Diwani wa Mlandege) na Eliud Mvella (Diwani wa Mkimbizi).

Eliud Mvela Mgombea umeya

Majina mapya ambayo yamezua mjadala, kwa mujibu wa taarifa hizo za wadau, ni pamoja na Amri Kalinga (Diwani wa Mkwawa), Thadeus Tenga (Diwani wa Makorongoni) na Galusi Lugenge (Diwani wa Mwangata).

Lakini mjumbe wa Kamati ya Siasa amezipinga vikali taarifa za kuwepo kwa upendeleo, akisisitiza kuwa zoezi hilo lilikuwa wazi, huru, na lililofuata utaratibu wa chama.


“Taarifa hizo si za kweli. Uchukuaji na urejeshaji fomu ulikuwa wa siku mbili, Novemba 20 na 21, na ulikuwa huru kwa kila diwani mwenye nia kamati inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba, kanuni na miongozo ya chama hakuna hatua inayofanyika kwa lengo la kumpendelea mtu,” alisema.

Amesema ni kawaida kwa michakato ya ndani ya chama kuibua hisia, mijadala, na wakati mwingine tuhuma, lakini amewataka wana-CCM kuwa na imani na mwenendo wa kamati.

“Wote waliochukua na kurudisha fomu ni madiwani wa CCM, na wote wana haki sawa mbele ya chama,” alisisitiza.

Kwa sasa, Kamati ya Siasa inaendelea na hatua za awali za mchujo, na macho ya wengi yapo kwenye orodha ya mwisho ambayo itaonesha ni nani atapenya na kuingia katika hatua inayofuata ya uchaguzi huo muhimu.

Matukio Daima Media kwa nyakati mbili tofauti jana Ijumaa Novemba 21  majira ya saa 11:40 jioni na leo majira ya 5:40 asubuhi amemtafuta katibu wa CCM wilaya ya Iringa mjini Hassan Makoba kutaka kujua idadi ya waliochukua fomu na madai ya kujaziwa fomu ambao hawakuchukua fomu ila jibu mara zote lilikuwa ni moja nipo kwenye kikao cha kamati ya siasa nitakupigia kisha anakata simu .

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI