NA MATUKIO DAIMA MEDIA, MOROGORO
Baraza la Usajili wa Biashara Tanzania (BRELA) limetoa zawadi ya shilingi laki tano kwa mwanafunzi bora wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kampasi ya Morogoro mwaka 2025 Melina Baradyana.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu BRELA, Afisa Habari Mkuu, Bi. Theresa Chilambo amesema zawadi hiyo ni matokeo ya ushirikiano baina ya BRELA na Chuo Kikuu cha Mzumbe, na inalenga kuhamasisha wanafunzi kufanya vizuri kitaaluma.
Amesema BRELA imeingia makubaliano na chuo kikuu Mzumbe yenye lengo kukuza bunifu za wananfunzi na wanajumuiya ya Mzumbe huku akisisitiza kuwa zawadi kama hiyo pia itatolewa kwa mwanafunzi atakayefanya vizuri katika kampasi za Dar es Salaam na Mbeya, akiwataka wanafunzi kuongeza juhudi zao ili kupata fursa kama hiyo.
Melina Baradyana, ambaye amehitimu Shahada ya Awali ya Usimamizi wa Mazingira, amesema zawadi hiyo imempa motisha kubwa ya kuendelea kufanya vizuri na kuwahamasisha wanafunzi wengine kuthamini masomo yao.
Alibainisha kwamba taaluma yake itamuwezesha kuchangia katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kupitia tafiti na ushirikiano na taasisi mbalimbali.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, ameishukuru BRELA kwa kutambua juhudi za wanafunzi na kusema kuwa Mzumbe inaendelea kujipanga kuwa chuo cha kimataifa kwa kuhamasisha ubadilishanaji wa wanafunzi na kuboresha mitaala kupitia ushirikiano na alumni, hatua ambazo zitaleta wahitimu wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo, Philemon Luhanjo, amewataka wanafunzi wapya kuwa na imani na Mzumbe, akisisitiza kuwa chuo hicho ni moja ya taasisi zinazozalisha viongozi na wataalamu mahiri nchini.








0 Comments