Header Ads Widget

ACT WAZALENDO WATISHIA KUIBURUZA MAHAKAMANI TUME HURU YA UCHAGUZI..

Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza mpango wa kuishtaki Mahakamani Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kikitaka kuzuia kuapishwa kwa wabunge wa viti maalum waliotangazwa hivi karibuni, sambamba na kuilazimisha tume hiyo kuweka wazi takwimu na vigezo vilivyotumika katika ugawaji wa viti hivyo.


Hatua hiyo imekuja baada ya INEC tarehe 7 Novemba 2025 kutangaza orodha ya wabunge wanawake wa viti maalum 115 walioteuliwa kushiriki katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kati ya hao, wabunge 113 wametoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wawili kutoka Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), huku ACT Wazalendo ikiwa miongoni mwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo lakini havikupata nafasi yoyote kwenye viti maalum.


Kwa mujibu wa taarifa ya INEC, idadi kamili ya wabunge wa viti maalum inapaswa kuwa 116, ambapo uteuzi wa nafasi moja umeahirishwa hadi kukamilika kwa uchaguzi wa majimbo ya Fuoni (Zanzibar) na Siha (Tanzania Bara).


Katika mkutano na wanahabari uliofanyika siku ya Jumapili, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, na Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa chama hicho, Janeth Rithe wamesema chama chao kimechukua hatua hiyo baada ya kubaini kasoro na ukiukwaji wa haki katika usimamizi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ambao wamesema umechafuliwa na vitendo vya uonevu, vifo, na ukiukwaji wa misingi ya kidemokrasia.


“Iundwe Tume Huru ya Uchunguzi nje ya serikali kuchunguza matukio yote yaliyosababisha kuvurugwa kwa uchaguzi mzima na wale waliohusika kwa makusudi wawajibike,” amesema Semu, akiongeza kuwa chama chake kinataka pia kuundwa kwa Tume ya Maridhiano ya Kitaifa (National Cohesion Commission) itakayowakutanisha serikali, viongozi wa vyama vya upinzani na wananchi kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa na kuweka mfumo bora wa uongozi wa kidemokrasia.


ACT Wazalendo imesema inaona haja ya mageuzi ya kikatiba yatakayounda Tume Huru ya Uchaguzi yenye mipaka iliyo wazi kati ya dola na chama tawala, pamoja na kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari na vyama vya siasa unalindwa kisheria.

                 

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI