Na Matukio Daima Media
MKUU wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi amewaonya wale wote watakaojaribu kuhamasisha ama kuleta uvunjifu wa amani wakati wa mchakato wa uchaguzi Mkuu hapo Oktoba 29, 2025 akitahadharisha wale wote wanaotaka kupandisha homa ya uchaguzi kutojaribu kufanya hivyo kwani watashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kanali Mtambi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 17, 2025 katika ukumbi wa Mwembeni Complex katika ufunguzi wa Mafunzo ya walimu kutoka mikoa minane ya Kanda ya ziwa na Kanda ya Magharibi, mafunzo yanayofanyika Mkoani humo, akiwahakikishia waalimu hao na wananchi wa Mkoa huo kuwa wamejipanga kikamilifu ,kuhakikisha kila mmoja anatumia haki yake ya kuchagua Kiongozi amtakaye katika mazingira tulivu na yenye amani na usalama wa kutosha.
"Huu ni mwaka wa uchaguzi na mwezi huu ndiyo hasa tumefika kunako sasa shughuli za kisiasa zimekuwa zikiendelea vizuri katika Mkoa wetu, Vyama vyote vimepata fursa sawa, Wagombea wamepata muda mzuri wa kunadi sera zao, Wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kusikiliza Wagombea kupitia Vyama mbalimbali, demokrasia Mkoa wa Mara imekua na inaendelea kupevuka."
"Naomba pia nitumie fursa hii kama Mwenyekiti wa Kamati ya usalama Mkoa, niwatanabaishe wale ambao wakati wa uchaguzi homa ya uchaguzi inapopanda inakimbilia kichwani na kuleta mfetuko wa vichwa, sasa vichwa vikifetuka wengine hufanya mambo yasiyokubalika, nitumie fursa hii kutoa onyo kwao, homa ya uchaguzi ikikupanda tafakari vizuri sera na itkadi ya Chama chako, usiniletee fujo katika Mkoa wa Mara na kama utajaribu utakutana na moto mkali kweli kweli na hapa sipepesi macho, hatutamvumilia yeyote atakayechafua hali ya hewa kwasababu tu amepata homa ya uchaguzi akaamua kujifanya kuwa kichaa, naomba asiwepo yeyote mwenye wazo la namna hiyo." Amesema Mhe. Mtambi.
Mtambi Alisema Mkoa wa mara Vyama vyote katika Mkoa huo vinaendelea kufanya kampeni zake za Amani na Utulivu suala linalotoa fursa ya ushiriki wa wananchi kwenye mikutano ya Kampeni kwa Vyama mbalimbali vya siasa katika Mkoa huo.
0 Comments