Na Matukio Daima Media
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Marco Chilya amethibitisha kupatikana kwa Padri Camillius Nikata wa Jimbo Kuu Songea na mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Agustino Mwanza, akisema kwamba Padri huyo hakutekwa kama ilivyoripotiwa kwenye Vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Chilya amesema Jeshi hilo katika uchunguzi wake lilifanikiwa kumpata Padri huyo kwenye mashamba ya Kijijini kwake Mawa, Kata ya Hanga Mkoani Ruvuma, akiwa amedhohofu kutokana na njaa bima ya jeraha lolote, akiwa na vitu vyote alivyoondoka navyo Jimboni ikiwa ni pamoja na begi lake la mgongoni, fedha, funguo na pesa shilingi 13, 500.
Kulingana na Kamanda Chilya, Padri Nikata aliamua kujipoteza mwenyewe kutokana na masuala yaliyokuwa yakimsibu, ikiwemo changamoto kwenye mahusiano yake ya Kimapenzi na msichana wa miaka 28 ambaye licha ya kumuhudumia Mamilioni ya pesa, msichana huyo aliachana na Padri Nikata mwanzoni mwa mwezi wa saba mwaka huu na kushindwa kurudiana kuendeleza mahusiano yao.
"Padri aliachwa na mpenzi wake aliyekuwa naye kwa takribani miaka tisa sasa, ambapo alikuwa akimuhudumia kwa gharama kubwa sana kabla ya kuachana ambapo katika Kipindi cha Mwezi Juni mpaka Septemba Padri huyo amemuhudumia Mpenzi wake huyo zaidi ya Milioni 39 akizitoa kwenye akaunti yake ya CRDB. Matumizi haya makubwa ya fedha yalimfanya mpaka kukosa fedha za kwenda kutibiwa jicho lake bahati mbaya zaidi Padri aliacha kazi na inaonekana hakupewa nafasi ya kusikilizwa na Uongozi wake." Amesisitiza Kamanda Chilya.
Sababu jingine iliyoelezwa na Kamanda Chilya kama chanzo cha Padri Nikata kujipoteza ni pamoja na msongo wa mawazo kutokana na wingi wa madeni yaliyokuwa yakimkabili ambapo upelelezi umeonesha kuwa alishindwa kuyalipa baada ya Jeshi hilo la Polisi kuwasiliana na waliokuwa wakimdai.
0 Comments