Header Ads Widget

NYALANDU AKUTANA NA VIONGOZI WA DINI KUHAMASISHA AMANI NA USHIRIKI KATIKA UCHAGUZI

 


Na Chausiku Said

Matukio Daima Media

Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameendelea na ziara yake mkoani Mara kwa kukutana na viongozi wa dini ili kujadiliana nao kuhusu nafasi yao katika kuimarisha amani na kuhamasisha waumini kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Tukio hilo limefanyika Oktoba 17, 2025, ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa ziara zake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambako amekuwa akikutana na makundi mbalimbali ya kijamii kuhimiza amani na umoja kuelekea uchaguzi mkuu.


Viongozi wa dini walioshiriki katika kikao hicho wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuitunza amani, hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi, na kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaoleta maendeleo katika kipindi kijacho cha miaka mitano.

Wamesema kumekuwepo na watu wanaoeneza taharuki miongoni mwa wananchi kuhusu zoezi la uchaguzi, hivyo serikali ina wajibu wa kuwalinda raia wake dhidi ya vitendo hivyo.

“Amani ni tunu pekee tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, hivyo Watanzania tunapaswa kulitambua hilo na kuendelea kuilinda kwa manufaa ya Taifa letu,” wamesisitiza viongozi wa dini.


Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Canal Evance Mtambi, amesema majukumu makuu ya vyombo vya ulinzi na usalama ni kulinda raia na mali zao, huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Awali, akizungumzia umuhimu wa kudumisha amani, Nyalandu alisema msingi wa umoja na mshikamano wa taifa ni jamii kuishi kwa upendo na ushirikiano, na akawahimiza viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu kwa waumini kuhusu umuhimu wa amani na ushiriki katika kupiga kura.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI