Na. Hance Mbena - Chato
"Ujirani mwema ni msingi wa ulinzi wa Maliasili na maendeleo endelevu".
Ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limeendelea kuwashukuru wateja wake wakiwemo makampuni ya utalii, wawekezaji na jamii kwa ujumla ambao wameendelea kuwa msingi wa uhifadhi na mapato kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali ndani ya taasisi na Taifa kwa ujumla.
Kutokana na umuhimu wa wiki hii jana, Oktoba 8, 2025, Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Rubondo imepokea wananchi zaidi ya 40 ambao ni miongoni mwa wateja wake wakuu waliojielekeza kufanya utalii wa ndani na kupata elimu ya uhifadhi wa maliasili ikiwemo ulinzi wa mazalia ya samaki. Wananchi hao ni kutoka katika kata tatu za wilaya ya Chato ambazo ni Muganza, Bwongera na Kigongo.
Mbali na kufanya utalii wa ndani na kupata elimu ya uhifadhi pia ziara hii ilijikita zaidi katika kuimarisha mahusiano kati ya hifadhi na jamii zilizoko pembezoni mwa hifadhi hii, pamoja na kujadili njia bora za kukuza ushirikiano uliopo baina ya pande hizi mbili ili kufikia lengo la uhifadhi endelevu wa maliasili na maendeleo ya jamii.
0 Comments