Waokoaji huko Java Mashariki, Indonesia wanakimbizana na muda ili kuwapata watu 38 wanaoaminika kuwa wamenasa kwenye vifusi vya jengo la shule ambalo lilianguka siku ya Jumatatu
Wanafunzi watatu wamefariki na wengine 99 walipelekwa hospitalini, baadhi yao wakiwa na majeraha mabaya, maafisa wanasema, na kuongeza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Wengi wa wale ambao wamenaswa ni wavulana ambao walikuwa wamekusanyika kwa maombi wakati jengo hilo lilipoanguka.
Jengo hilo la ghorofa mbili lilikuwa na msingi usio imara na halikuweza kuhimili uzito wa ujenzi wa ziada wa ghorofa mbili zaidi, maafisa wanasema.
Waokoaji wanajaribu kuwafikia manusura walionaswa chini ya kifusi - ambao baadhi yao bado wanaitikia - wakati familia zinasubiri kwa wasiwasi habari za wapendwa wao.
Maafisa wanasema kuna maeneo ambayo bado wanawasiliana na manusura - na wamewapa oksijeni, chakula na maji.
Operesheni ya uokoaji ilisitishwa kwa muda Jumanne, baada ya mamlaka kuonya juu ya jengo hilo kuanguka zaidi.
Wanafunzi walikuwa wamekusanyika kwa maombi katika Shule ya Bweni ya Kiislamu ya Al Khoziny, katika mji wa Java Mashariki wa Sidoarjo, wakati jengo hilo lilipoporomoka.
Mamlaka inasema shule hiyo haikuwa na vibali vya kupanua jengo lake.






0 Comments