Header Ads Widget

WANNE WAFARIKI KWA AJALI YA BARABARANI SONGWE.

 

NA MATUKIO DAIMA MEDIA.

SONGWE.Polisi Mkoani Songwe imeripoti kutokea kwa ajali mbili tofauti ambapo katika ajali ya kwanza ilitokea mnamo Septemba 29, 2025, majira ya saa 5 usiku katika eneo la Hanseketwa, Kata ya Ihanda, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, kwenye barabara kuu ya Tunduma Mbeya.

Akitoa taarifa kwa umma, Kamanda wa Polisi mkoa wa Songwe kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Augustino Senga, amesema ajali ya kwanza ilihusisha gari lenye namba za usajili T.908 CSV aina ya Toyota IST, rangi ya silver lililokuwa likiendeshwa na Musa Njowela Elton (38) fundi ujenzi na Mkazi wa Tunduma Wilaya ya Momba ambaye alikuwa anatoka katika kijiji cha Shiwinga kuelekea Tunduma.

Amesema gari hilo liligonga kwa nyuma ubavuni mwa tela la gari lenye namba za usajili T.758 AQP/T.704 AKH, aina ya Scania, mali ya Arafat Razac Ladha lililoegeshwa upande wake wa barabara baada ya kupata itilafu lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Tunduma na kusababisha vifo vya watu wawili, ambao ni Queen Watson Sampamba (36) na Wasi Berdon Mgalla (42) wafanyabiashara, wakazi wa Tunduma Wilayani Momba.

Aidha, katika ajali hiyo Dereva wa gari dogo, Musa Njowela, aliumia sehemu mbalimbali za mwili wake na anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi, huku magari yote mawili yakiwa yameharibika vibaya.

Kamanda Senga amesema baada ya ajali hiyo, dakika chache zisizozidi 5 katika eneo hilohilo ilitokea ajali nyingine iliyohusisha gari lenye namba za usajili T.425 EEV aina ya Toyota Surf, yenye rangi nyeusi, lililokuwa likiendeshwa na Abdul Lugano Mwakapesa (50), mfanyabiashara, Mkazi wa Mpemba Wilaya ya Momba ambaye alikuwa anatoka Wilaya ya Kyela kuelekea Tunduma.

Polisi inasema gari hilo liligonga kwa nyuma tela la gari lile lile la Scania (T.758 AQP/T.704 AKH) lililokuwa limehusika kwenye ajali ya kwanza na kusababisha vifo vya watu wawili na majeruhi wanne. 

Amesema kwenye ajali hiyo, waliofariki ni Emmanuel John Mwangemile (55) mfanyabiashara na Emmanuel Martin Kandonga (50), Afisa Elimu Kata ya Mpemba wote wakazi wa Mpemba Wilaya ya Momba na majeruhi waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Winfrida Bakari Mwandule (30),  Merisenti John Kimpa (41), Suzie Mwakabonga (28), Elisha Matata Sindwani (30), wote wafanyabiashara na wakazi wa Mpemba Wilaya ya Momba.

Majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe na chanzo cha ajali hiyo kinatajwa kuwa ni mwendokasi ambapo dereva wa gari la Toyota Surf, Abdul Mwakapesa, alikimbia mara baada ya tukio hilo na Polisi Mkoa wa Songwe inaendelea na msako mkali ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa madereva wote wanaotumia barabara kuu ya Tunduma Mbeya na barabara nyinginezo kuwa makini, kuzingatia sheria, alama na michoro ya usalama barabarani na kuepuka uzembe wa kuendesha kwa mwendo kasi ili kuepuka ajali zinazosababishwa na kukosa umakini.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linawakumbusha madereva kuacha tabia ya kukimbia baada ya ajali, kwani ni kosa la jinai na hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka sheria za usalama barabarani.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI