Na Farida Mangube, Morogoro
Tafiti za kilimo zinazotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) zimeendelea kuwa chachu muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula, na ukosefu wa ajira kwa vijana nchini.
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa tuzo kwa wanafunzi na watumishi waliofanya vyema katika masomo, utafiti na ubunifu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, alisema utaratibu huo ni ishara ya safari ndefu ya umahiri, ubunifu na kujituma unaoendelea kukipambanua SUA kama chuo kinachoongoza katika mageuzi ya sekta ya kilimo.
“Elimu ya kilimo lazima iwe ya vitendo na iwe inatatua changamoto halisi za maisha kama ukosefu wa chakula, mabadiliko ya tabianchi, na ajira vijijini,” alisema Bw. Mweli.
Aliongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo BBT, SUA STEPS, na Agricultural Innovation Program (AIP), inayolenga kuwajengea uwezo vijana na kubadilisha kilimo kuwa biashara endelevu yenye faida.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema zaidi ya wanafunzi na watafiti 180 wamefanya vizuri katika masomo, tafiti na ubunifu mbalimbali, na watatunukiwa zawadi kuanzia shilingi elfu 50 hadi milioni moja.
Prof. Chibunda aliwapongeza washindi hao na kueleza matumaini yake kwamba wataendelea kutumia maarifa yao kutatua changamoto zinazolikabili taifa.
“Tafiti nyingi zinazofanywa SUA zinalenga kuongeza tija ya uzalishaji, kudhibiti magonjwa ya mimea na mifugo, kuhifadhi mazao baada ya mavuno, na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali maji,” alisema Prof. Chibunda.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Maulid Mwatawala, alisema utaratibu wa chuo cha kuwazawadia wanafunzi na wanataaluma wanaofanya vizuri ni kichocheo muhimu cha kuongeza ari na ufanisi katika masomo, utafiti na ubunifu.
“Kutambua juhudi za wanafunzi na watafiti kunaleta ushindani chanya na kuimarisha ubora wa elimu na tafiti zinazofanyika chuoni,” alisema Prof. Mwatawala.
0 Comments