Header Ads Widget

SERIKALI YATANGAZA ELIMU YA LAZIMA MIAKA 10, WADAU WAIUNGA MKONO

Na Hamida Ramadhan Matukio DaimaMedi Dodoma

SERIKALI imetangaza rasmi mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuongeza muda wa elimu ya lazima kutoka miaka saba hadi kumi, ikijumuisha elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, ameyasema hayo jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa tathmini ya pamoja ya sekta ya elimu, ambapo amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa sawa ya kujifunza na kupata ujuzi wa maisha.


 “Hii ni hatua ya kimkakati itakayowezesha taifa kujenga kizazi chenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali na viwanda,” amesema Prof. Mushi.

Amesema utekelezaji wa sera hiyo mpya utahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, jamii, na wadau wa elimu, hasa katika kuongeza miundombinu, walimu na vifaa vya kujifunzia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Simon Nanyaro, amepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa wadau wako tayari kusaidia serikali katika utekelezaji wake.


“Mageuzi haya yanahitaji nguvu ya pamoja. Tumejipanga kufanya uwekezaji mkubwa kwenye elimu ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi sawa ya kujifunza,” amesema Nanyaro.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka, amesema mradi wa HEET unaotekelezwa na serikali utaimarisha zaidi elimu ya amali na kukuza ubunifu miongoni mwa vijana.

 “Kupitia HEET, vyuo vyetu vinapata fursa ya kuboresha miundombinu na programu za ubunifu ambazo zitawajenga wanafunzi kuwa wabunifu na wabunifu wa suluhisho kwa jamii zao,” amesema Prof. Kusiluka.

Mussa Buluki, mwakilishi wa BASUTA, naye ameahidi kuwa taasisi yake itaendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha ubora wa elimu nchini.


Naye wanafunzi, Rehema James Mgala, kutoka Shule ya Sekondari Kisasa, amesema elimu ya amali imewasaidia kujitegemea na kuanzisha miradi midogo ya ubunifu.

“Tunachojifunza darasani tunakitumia hata nyumbani. Tunatengeneza bidhaa ndogo ndogo zinazotuletea kipato,” amesema Rehema kwa furaha.


Mkutano huo wa siku tatu, uliohudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali za elimu, vyuo vikuu na mashirika ya maendeleo, umebeba kaulimbiu “Mageuzi ya Elimu kwa Maendeleo Endelevu.”

Kupitia maazimio yake, serikali inalenga kuimarisha mfumo wa elimu utakaomjenga kijana wa Kitanzania kuwa na maarifa, ujuzi na maadili yanayohitajika katika dunia ya sasa.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI