Na Hadija Omary
Lindi — Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Salma Rashid Kikwete, ameendelea na kampeni zake za kuomba kura kwa wananchi wa jimbo hilo, huku akiahidi kusimamia mchakato wa kugawa maeneo ya kiutawala kwa lengo la kulifanya Jimbo la Mchinga kupata hadhi ya halmashauri kamili.
Katika mikutano yake iliyofanyika katika vijiji vya Legezamwendo na Mkangaulani, Kata ya Milola, Bi. Salma aliweka wazi kuwa kuanzishwa kwa halmashauri hiyo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Mchinga.
Wakati huo huo, Mgombea Udiwani wa Kata ya Milola, Hassan Kimbyoko, aliwahamasisha wananchi kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi zote za uongozi, akieleza kuwa zaidi ya shilingi bilioni moja zimetolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.
Wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walionesha imani na matumaini kwamba Bi. Salma ataendeleza juhudi za kuwaletea maendeleo, huku wakibainisha kuwa changamoto ya barabara katika baadhi ya maeneo inapaswa kupewa kipaumbele mara baada ya uchaguzi.
0 Comments