Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amepanga kufanya "mazungumzo ya kitaifa" na makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wawakilishi wa vijana, na viongozi wa kiroho katika ikulu yake baadaye mchana wa leo kwa saa za nchini humo.
Mazungumzo haya yanafuatia mfululizo wa mikutano aliyoifanya mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kuwasikiliza zaidi wananchi.
Jana usiku, aliteua mawaziri watatu wa baraza la mawaziri, wa Ulinzi, Usalama wa Umma, na Mjumbe wa Waziri anayesimamia polisi, kufuatia uteuzi wa awali wa Waziri Mkuu mpya.
Rais huyo anayekabiliwa na mzozo anaonekana kufanya kila kitu isipokuwa kutii matakwa ya waandamanaji vijana, ambao wamekuwa wakiandamana kwa zaidi ya wiki mbili.
Siku ya Jumanne, vijana waandamanaji walitoa makataa ya saa 48 kwa rais kutimiza matakwa yao la sivyo akabiliane na mgomo wa nchi nzima.
Lakini rais ameendelea kusisitiza umoja na haja ya kulinda nchi dhidi ya machafuko.
"Pamoja, lazima tuungane kupigana dhidi ya maovu haya na kujenga jamii mpya iliyosimikwa katika mshikamano na kuheshimiana," aliandika Rajoelina jana kwenye ukurasa wa Facebook wa ofisi yake.
Baadhi ya raia wa Madagascar wameambia BBC kwamba ingawa wanaunga mkono malalamiko ya vijana hao, wana wasiwasi kwamba maandamano ya muda mrefu yanaweza kudhuru maisha yao.
"Ninamuunga mkono kikamilifu Gen Z, lakini sidhani kama maandamano ndiyo njia sahihi ya kushughulikia malalamiko yao. Watu wanapoandamana, siwezi kufanya biashara," anasema Laza Brenda, ambaye anaendesha kioski cha kutengeneza simu za mkononi kando ya barabara.
Mjasiriamali Ulrichia Rabefitiavana anasema baadhi ya wateja wake wa kimataifa wameghairi kandarasi za mafunzo na hafla za semina ambazo kampuni yake ilikuwa ikisimamia kutokana na kutokuwa na uhakika uliosababishwa na maandamano.
Wakati Rajoelina akiendelea kupuuza wito wa kujiuzulu, na vyama vya upinzani vikishiriki zaidi katika maandamano yanayoongozwa na vijana, wengi wanahofia mzozo wa kisiasa unaoendelea utazidi kuwa mbaya katika siku zijazo.
0 Comments