Header Ads Widget

RAIS WILLIAM RUTO ATANGAZA MAOMBOLEZO YA KITAIFA KWA HESHIMA YA RAILA ODINGA

 

Rais William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga.

Katika kipindi hiki, bendera zote za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya heshima na maombolezo.

Aidha, Rais Ruto ametangaza kusitisha shughuli zake zote za umma na kuwasihi maafisa wengine wa serikali kuchukua hatua kama hiyo ili kutoa nafasi ya kutafakari na kuomboleza maisha ya kiongozi huyo mashuhuri.

Kwa ajili ya maandalizi ya mazishi ya kitaifa, Rais ametangaza kuundwa kwa kamati maalum ya kushughulikia shughuli hizo, itakayokuwa chini ya uongozi wa Naibu Rais Kithure Kindiki.

Serikali ya India, kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Kenya, imeahidi kugharamia na kuratibu shughuli za kusafirisha mwili wa marehemu kutoka India hadi Kenya kwa ajili ya mazishi.

Wakati huo huo, ujumbe wa viongozi wakuu wa serikali, ukiongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Mheshimiwa Musalia Mudavadi, unaondoka nchini Kenya kuelekea India haraka iwezekanavyo ili kushughulikia mipango ya mwisho ya usafirishaji wa mwili wa marehemu.

Rais Ruto amemsifu marehemu Raila Odinga kama mtu asiye na tamaa ya makuu, mpenda amani, na mzalendo wa kweli.

“Raila alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyejitolea kwa dhati kwa ajili ya taifa hili. Alisimamia haki, usawa na amani. Ni shujaa ambaye historia haitamsahau,” alisema Rais Ruto.

Mazishi ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika katika siku zijazo, huku taifa likiendelea kuomboleza mmoja wa viongozi wake wakuu waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya demokrasia na haki za Wakenya.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI