Na Shemsa Mussa -Matukio Daima Media
Missenyi, Kagera
Mgombea wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezungumza na Wananchi katika kata ya Kyaka, Wilaya ya Missenyi, ambapo ameeleza dhamira ya serikali kuendelea kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya miundombinu, elimu, afya, na kilimo.
Dkt. Samia ametangaza utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 23, unaolenga kuhudumia wakazi wa kata mbalimbali za Missenyi. Mradi huo unatarajiwa kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya vijijini na mijini.
Kwa upande wa sekta ya afya, Dkt. Samia amesema serikali imetenga shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya pamoja na ununuzi wa magari matatu ya wagonjwa. Aidha, ameahidi kujengwa kwa barabara mbili kuanzia Bulembo Kona hadi hospitali ya wilaya, ili kurahisisha usafiri wa wagonjwa na huduma nyingine za afya.
Katika sekta ya elimu, serikali imetenga shilingi bilioni 7.2 kwa ajili ya kuendeleza mpango wa elimu bila malipo. Hili ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora na ya msingi bila vikwazo vya kifedha.
Kuhusu masuala ya kilimo, Dkt. Samia ameeleza kuwa miche milioni 2 ya kahawa na miche laki tano ya parachichi itasambazwa kwa wakulima ili kuongeza tija na kipato. Aidha, serikali imeahidi kujenga soko kubwa katika eneo la Bunazi , pamoja na ujenzi wa jengo la abiria katika soko dogo la Ndizi ili kuboresha biashara na shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Vilevile, amebainisha kuwa minara nane ya mawasiliano itajengwa katika maeneo ya Kasambya, huku upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kyaka ukiwa kwenye mpango wa haraka. Pia, serikali imepanga kutumia shilingi bilioni 54 kukamilisha ujenzi wa barabara muhimu katika wilaya hiyo. Uwanja wa ndege Wa Kagera sugar utaboreshwa ili kuweza kubeba abiria 180 kwa wakati mmoja, hatua itakayowezesha ukuaji wa uchumi wa utalii na usafiri wa anga kwa wakazi wa mkoa wa Kagera.
0 Comments