Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA cha Wafanyakazi wa Hoteli, Majumbani, Hospitali na Taasisi Zinazotoa Huduma za Afya Tanzania (CHODAWU) kimesema uridhiaji wa Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 189 ni hatua muhimu katika kuimarisha ulinzi wa haki za wafanyakazi wa majumbani nchini.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Said Wamba, amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa kazi, wafanyakazi wa majumbani bado wanakabiliwa na changamoto zinazohitaji maboresho ya kisera na kisheria.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Kazi za Majumbani wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30 uliofanyika jijini Dodoma, Wamba amesema kundi hilo bado linakumbwa na mishahara isiyoendana na kazi wanazofanya, ukosefu wa mikataba rasmi ya ajira na mazingira yasiyo salama ya kazi.
Amesema uridhiaji wa mkataba huo utaongeza nguvu katika kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani na kuweka misingi imara ya kazi zenye staha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani nchini, Zanini Athumani, amesema baadhi ya wafanyakazi wa majumbani huendelea kufanya kazi kwa saa nyingi bila utaratibu mzuri wa mapumziko huku wengine wakikosa njia za kufuatilia haki zao wanapokumbana na migogoro ya kikazi.
Aidha, ameeleza kuwa mawakala wa ajira wasiokuwa rasmi wameendelea kuwa chanzo cha malalamiko kutokana na vitendo vya unyonyaji vinavyoripotiwa na baadhi ya wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la CVM, Laura Vallesi, amesema wanawake na watoto bado ni miongoni mwa makundi yanayoathiriwa zaidi na changamoto zilizopo katika sekta ya kazi za majumbani.
Amesema baadhi ya watoto huondolewa katika mazingira yao kwa ahadi za kupata elimu na maisha bora lakini huishia kufanya kazi katika mazingira yasiyolinda ustawi wao.
Naye Meneja Miradi wa Shirika la Wote Sawa, Jackline Mujunangoma, amesema kuna haja ya kuongeza juhudi za kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu unaowaathiri wanawake na wasichana wengi.
Amesema mashirika ya kiraia yanaendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa msaada kwa waathirika na kuhamasisha jamii kutambua na kuripoti vitendo vya unyonyaji.
Wadau waliohudhuria mkutano huo wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, vyama vya wafanyakazi, waajiri na mashirika ya kiraia katika kuhakikisha wafanyakazi wa majumbani wanapata haki, usalama na mazingira bora ya kazi.
Mwisho









0 Comments