Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi wapya katika taasisi zinazosimamia huduma za mabasi yaendayo haraka jijini Dar es salaam.
Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt Moses Kusiluka imeeleza kuwa, Sais Tunda ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART).
Tunda anachukua nafasi ya Dkt Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Pia Rais Samia amemteua Pius Ng’ingo kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi yaendayo haraka (UDART), akichukua nafasi ya Waziri Kindamba ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa.
Hapo jana picha za video zilisambaa mitandaoni zikionesha baadhi ya vioo vya mabasi na vituo vikiwa vimevunjwa baada ya kushambuliwa kwa mawe usiku wa kuamkia leo Jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni njia hiyo ya usafiri inayotegemewa na maelfu ya wakazi wa jiji hilo kubwa zaidi nchini Tanzania imekumbwa na malalamiko ya wananchi kutokana na uhaba wa mabasi ikilinganishwa na idadi ya abiria.
Hata hivyo jumatano asubuhi mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo kikuu cha mabasi ya mwendo kasi na kuwaomba radhi watumiaji wa usafiri huo na kuwataka kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na mipango ya kutatua adha wanazozipitia ikiwemo kuongeza idadi ya mabasi.






0 Comments