Header Ads Widget

NYOMI KATIKA MIKUTANO YA KAMPENI YA LUKUVI ISIMANI YAONEKANA KUWA USHINDI MKUBWA KWA DKT. SAMIA


Na Matukio Daima Media
Isimani, Iringa

Wimbi kubwa la wananchi wanaohudhuria mikutano ya kampeni ya mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. William Vangimembe Lukuvi, limeendelea kuonyesha taswira ya wazi kwamba Chama Cha Mapinduzi na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga imani kubwa kwa wananchi. 


Nyomi ya watu wanaohudhuria mikutano hii imekuwa ikiongezeka kila siku, jambo linalotafsiriwa kuwa ni ishara ya mapokezi makubwa ya sera za maendeleo za CCM na uungwaji mkono kwa Dkt. Samia 2025.

Katika mikutano iliyofanyika katika kata za Ilolo Mpya, Mlenge, Itunundu na Mboliboli ndani ya Tarafa ya Pawaga, umati mkubwa wa wananchi umejitokeza kushiriki, kusikiliza sera na kutoa maoni yao kuhusu maendeleo ya jimbo. Nyomi hiyo siyo tu kwamba imeashiria mwitikio mkubwa wa kampeni, bali pia imeonesha mshikamano wa wananchi katika kuunga mkono juhudi za kiongozi wao aliyelitumikia jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 25, Mhe. Lukuvi.

Wananchi wameonekana kufurahishwa na mwenendo wa kampeni za CCM zinazoongozwa kwa utulivu, hoja na mikakati yenye kujibu mahitaji ya wananchi wa Isimani, hususan katika maeneo ya miundombinu, kilimo, afya, elimu na maji. Katika hotuba zake, Mhe. Lukuvi amekuwa akisisitiza kuwa dhamira yake ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Dkt. Samia katika kuharakisha miradi ya kimkakati inayolenga kuinua uchumi wa wananchi wa Isimani.

Akizungumza mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa Ilolo Mpya, Lukuvi alisema:

“Isimani inakwenda kuwa kitovu cha uchumi kwa mkoa wa Iringa. Tunayo fursa ya ardhi yenye rutuba, tunayo mito ya umwagiliaji na tunayo nguvu kazi ya vijana. Jukumu letu ni kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita ili kuhakikisha kilimo kinakuwa biashara inayolipa, barabara zinapitika na huduma za kijamii zinaboreshwa.”

Katika mikutano hiyo, kauli mbiu ya maendeleo imekuwa ikisisitizwa, huku wananchi wakiendelea kuonyesha imani kuwa CCM ndiyo chama pekee chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo nchini. 


Huku wananchi wakimpa matumaini makubwa Lukuvi  kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia kuleta mageuzi katika sekta za elimu, afya na uchumi, wakieleza kuwa kasi yake katika kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati imewapa matumaini mapya.

Aidha, viongozi wa chama na makada walioambatana na Lukuvi katika mikutano hiyo wameendelea kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo uchaguzi mkuu, ili kusimamia maendeleo yaliyoanza chini ya uongozi wa CCM yasirudi nyuma.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, katika hotuba yake, alisema:

“Kila mkutano una nyomi, hii ni ishara kwamba wananchi wa Isimani wameamua. Wameamua kuendelea na chama chenye dira ya maendeleo. Hawa ni watu wanaotambua thamani ya uongozi wa Dkt. Samia na wanatambua mchango wa Lukuvi katika kuwatumikia.”

Wakati huo huo, vijana na wanawake wa Isimani wameonekana kujitokeza kwa wingi katika kampeni hizo, jambo ambalo limeitafsiriwa kuwa ni kielelezo cha kuongezeka kwa ushiriki wa makundi hayo katika masuala ya kisiasa na maendeleo. Vijana wengi walihojiwa walisema wanamkubali Lukuvi kwa sababu ni kiongozi anayetekeleza na si wa maneno pekee.

kampeni za Mhe. Lukuvi katika Jimbo la Isimani zimeendelea kuonesha nguvu kubwa ya kisiasa ya CCM katika mkoa wa Iringa na kuibua mjadala mpana kwamba nyomi hizi za wananchi ni ishara ya kushindwa mapema kwa wapinzani kabla ya kura kupigwa. Wananchi wengi wamepatikana wakitamka kauli moja: “Safari ya Maendeleo inaendelea – ni kazi iendelee!”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI