Header Ads Widget

NCAA YATAKIWA KUWEKA JITIHADA ZA KUSHIRIKISHA JAMII KWENYE SHUGHULI ZA UHIFADHI.

 




Na,Jusline Marco :Arusha

Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka wizara ya maliasili na utalii kupitia bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya Mamlaka ya hifadhi ya ngorongoro kuhakikisha miundombinu ya jengo la makumbusho ya kisasa ya jiolojia Ngorongoro - Lengai linatunzwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.


Dkt. Mpango ametoa wito huo katika uzinduzi wa jengo hilo lililopo Wilayani Karatu Mkoani Arusha ambapo amesema ni muhimu kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha ukarabati na matengenezo ya mara kwa mara ya miundombinu na mifumo iliyowekwa katika jengo hilo.

Aidha ameitaka NCAA kufanya jitihada za makusudi kushirikisha jamii inahoizunguka eneo hilo katika shughuli za uhifadhi wa eneo hilo zikiwemo mila, desturi na tamaduni zake ambapo pia amewataka watanzania kujenga utamaduni wa kutembekea vivutio na maeneo ya kihistoria ili kujifunza na kujionea utajiri wa nchi.

Uzinduzi huo umefanyika Oktoba 16 ,2025 baada ya mradi huo kukabidhiwa na serikali ya China kwa serikali ya Tanzania ambao umegharimu fedha za kitanzania shilingi bilioni 32 ambazo ni msaada kutoka serikali ya jamhuri ya watu wa china ambao ulilenga kuboresha miundombinu ya utalii,ujenzi wa makumbusho ya kisasa ya jiolojia na kuendeleza shughuli za uhifadhi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi ya jiolojia ya Ngorongoro-Lengai

Dkt. Mpango amesema Tanzania kupitia eneo la hifadhi ya Ngorongoro ilipewa hadhi ya kuwa eneo lenye utalii wa Miamba mwaka 2018 na kuwa Geopark pekee katika nchi za kusini mwa jangwa la sahara naya pili kwa Afrika ambapo amesisitiza kuwa kukamilika kwa makumbusho hayo kutavutia wageni kutembelea na kupata taarifa za jiolojia.

Ameongeza kwa kusisitiza kuwa uendeshaji wa mradi huo mpya kuenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumishi watakaohudumia wageni watakaotembelea makumbusho hayo,kutunza na kuboresha miundombinu,kusaidia na kushirikisha jamii inayozunguka eneo la hifadhi ya Ngorongoro.

Vilevile amesisitiza suala la utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kuwa linapaswa kupewa kipaumbele katika uendelezaji na utunzaji utalii ili kuepukana na kuvurugika kwa ikolojia na hatari dhidi ya ustawi wa shughuli za utalii ambapo amesema kutokana na uharibifu wa mazingira,inashuhudiwa muingiliano kati ya wanyamapori na binadamu unaopelekea athari kubwa zaidi vikiwemo vifo na uharibifu wa makazi na mazao.

Kwa upande wake  Balozi wa China nchini Tanzania Mhe. Chem Mingjian katika hafla hiyo amesema kuwa mradi huo ni wa aina yake barani Afrika chini ya mpango wa Belt and Road Initiative kwani unadhihirisha ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Tanzania ulioanza tangu mwaka 1964.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema eneo hilo pamoja na kuwa na hadhi ya Geopark, pia limeshinda tuzo ya kuwa kivutio cha utalii Barani Afrika mwaka 2023 na 2025 kupitia mtandao wa World Travel Awards.

Awali Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Venance Mabeyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro akizungumza katika uzinduzi huo amesema uboreshaji wa miundombinu ya utalii ni nguzo muhimu katika kukuza sekta hiyo na kuvutia watalii zaidi.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI