Header Ads Widget

MKOMI: MABARA ZA WAFANYAKAZI NI MUHIMU KUIMARISHA MAHUSIANO KAZINI


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima  Dodoma

KATIBU Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, amesema uanzishwaji wa mabaraza ya wafanyakazi mahali pa kazi ni sehemu ya utekelezaji wa haki ya ushirikishwaji wafanyakazi na kufikia malengo ya kuboresha maslahi na mahusiano mazuri kati ya wafanyakazi na waajiri katika maeneo ya kazi.

Akizungumza jana jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza la Nane la Wafanyakazi cha siku mbili, Mkomi alisema uanzishwaji wa mabaraza hayo ni utekelezaji wa kifungu cha 74(1), (2) na (3) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura Namba 366 pamoja na Kanuni 107 ya Kanuni ya Utumishi wa Umma za mwaka 2022.

Mkomi amefafanua kuwa uanzishwaji wa mabaraza hayo unatokana na matakwa ya kisheria kwa madhumuni ya kuishauri serikali na waajiri katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo usimamizi wa rasilimali watu.

"Baraza hili ni jukwaa muhimu mahali pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na wafanyakazi waliopo katika wizara hii ni matumaini yangu jukwaa hili litatumika kuishauri wizara katika utekelezaji wa majukumu yake, kusimamia maslahi, haki na ustawi wa wafanyakazi," alisema.

Katika hatua nyingine, Mkomi amewasihi Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mifumo ya kielektroniki ya kusimamia utumishi wa umma wa usimamizi wa utendaji kazi (PEPMIS), na mfumo wa usimamizi wa utekelezaji wa mradi (PIMS).

Amesema kuwa wafanyakazi watakaoshindwa kutimiza takwa hilo hawatastahili kupandishwa vyeo huku akieleza kuwa mifumo hiyo ikitumika vizuri itarahisisha utoaji wa huduma kwa wateja na wananchi.

"Najua ni mfumo mgeni, wengi wetu hatuupendi, unakuja kutubana, lakini niwahamasishe kwamba mifumo hii imeletwa kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi," alisema.

Akizungumzia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, Mkomi alisema, "Mimi sina chama lakini nina mapenzi na watu fulani niwahamishe watumishi wenzangu kwenda kushiriki kwenye uchaguzi kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura."

Ameongeza kuwa wanasiasa na mashujaa wanahamasisha watu kujitokeza kupiga kura na familia zao, huku akiwaomba wajumbe wa baraza hilo ifikapo Oktoba 29 waende kupiga kura.

Kuhusu kampeni ya Mama Samia Legal Aid, ameeleza kuwa anamini wajumbe wa baraza hilo watajadili namna ya kuboresha utendaji wa kitengo hicho, huku akisema kitengo hicho kinakimbiliwa na watu huko mitaani wakiamini wanakwenda kupata suluhu ya matatizo yao.

"Hivyo niwaombe wenzetu wanaosimamia kitengo hiki waendelee kusimamia kwa ukaribu ili tuone matunda yanayotarajiwa kutoka kwenye kitengo hiki," amesema.

Awali, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema kuwa lengo la baraza hilo ni kuwawezesha kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji na utekelezaji wa mipango ya wizara hiyo, pamoja na changamoto ambazo wanakutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kikao hicho ni maalum kwa ajili ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2024/2025 ambao pia unalenga kupima mafanikio ya shughuli za wizara hiyo na kupata taarifa ya bajeti iliyopitishwa ya 2025/2026.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI