Na Hamida Ramadhani, Matukio Daima.
_Agusia tatizo la ukosefu wa Ujuzi kwa wahitimu_
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) na Mkaguzi Mkuu mstaafu wa hesabu za serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad, amesema hali ya uchumi wa Tanzania kwa sasa kwa miaka hii minne ya serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni nzuri ukilinganisha na miaka ya nyuma, huku ukuaji wa uchumi ukiendelea kwa kasi na mfumuko wa bei ukiwa katika viwango vinavyoridhisha.
Akizungumza na waandishi wa habari kando ya Kongamano la Kitaaluma la kujadili Utekelezaji wa Uchumi Jumuishi kuelekea Dira 2050, lililoandaliwa na MUM kwa ushirikiano na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Profesa Assad amesema uchumi wa nchi umekua kwa wastani wa asilimia 6 katika kipindi cha miaka minne iliyopita suala ambalo limesaidia watanzania kuendelea kupata mahitaji yao muhimu kama Vyakula, elimu ma mahitaji mengine.
“Kwa jumla uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia sita. GDP, kupanda na kushuka kwa pato la taifa kumekaa vizuri ukilinganisha na nchi jirani. Hali ya kiuchumi ni nzuri zaidi kuliko Kenya na Rwanda,” amesema Profesa Assad.
Profesa Assad amesema kuwa vigezo vya kiuchumi vya sasa vinaonyesha uwezo bora zaidi wa wananchi kuendesha maisha yao ukilinganisha na miaka ya nyuma, jambo linalodhihirisha uimara wa uchumi wa nchi.
Aidha Profesa Assad ameeleza kuhusu changamoto ya vijana wanaohitimu vyuo vikuu kukosa ujuzi wa vitendo, akibainisha kuwa tatizo siyo kutokuwa sehemu ya uchumi, bali kukosa stadi za kazi, akisema Vijana wanaotoka Vyuoni wanapaswa kupewa mafunzo ya ujuzi kwa vitendo baada ya kumaliza masomo akisema jambo hili linapaswa kubebwa na serikali na sekta binafsi kwa kutoa kozi na fursa fupi za Vijana hao kujifunza zaidi kwa vitendo masuala mbalimbali ili kupata ujuzi.
0 Comments