Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha Mhe. Dkt. Lameck Ng'ang'a Karanga, amewahakikishia usalama na mazingira tulivu wananchi wote wa Wilaya hiyi katika Kipindi cha lala salama cha Kampeni za Uchaguzi Mkuu, wakati wa Upigaji kura na hata baada ya Mchakato huo kukamilika, akiwataka wananchi kupuuza Taarifa za Mitandaoni za kutokuwa na uchaguzi Jumatano Ijayo Oktoba 29, 2025.
Dkt. Karanga ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake akisisitiza pia wapigakura wote kurejea Majumbani mara baada ya kukamilisha zoezi la Upigaji wa kura na kuachana na baadhi ya hamasa zinazofanywa kwenye Mitandao ya Kijamii kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wanaohamasisha wafuasi wao kusalia vituoni kulinda kura suala ambalo ni jukumu la Polisi na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi nchini Tanzania.
Kwa upande wake Bi. Farida Kimambo, Msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Karatu, ameeleza kuwa maandalizi ya uchaguzi Mkuu 2025 yamekamilika, akisema vituo vya kupigia kura ni vile vilivyotumika kujiandikishia, akiwataka wananchi kufika sasa kwenye Vituo hivyo kuhakiki Taarifa na Majina yao.
"Mpigakura ambaye kitambulisho chake kimepotea ama kuharibika anaweza kupiga kura kwa kutumia leseni ya udereva, pasi ya kusafiria au kitambulisho cha NIDA ili aweze kupiga kura lazima awe amejiandikisha kwenye daftari la mpigakura na lazima jina alilojiandikishia liwe limefanana na Jina la kwenye Kitambulisho, leseni au pasi yake ya kusafiria." Amesema Msimamizi huyo wa uchaguzi.
Bi. Kimambo pia ameeleza kuwa Oktoba 25, 2025 watakuwa na semina ya mafunzo kwa makarani waongoza wapigakura kura kwenye Vituo vya Kupigia kura na Oktoba 26 na 27 watafanya mafunzo mengine kwa wasimamizi wa Vituo na wasaidizi wasimamizi wa Vituo ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa pamoja na kuyafahamu majukumu yao wakati wa zoezi la upigaji kura hapo Oktoba 29, 2025.





0 Comments