Header Ads Widget

MAMLAKA ZA UGANDA ZAKANUSHA KUWASHIKILIA WANAHARAKATI WA KENYA


Mamlaka ya Uganda imekanusha kuwashikilia wanaharakati wawili wa Kenya wanaodaiwa ‘kutekwa nyara’ jana Jumatano katika mji mkuu Kampala.

Mwanasiasa mkuu wa upinzani Bobi Wine ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi Ssentamu kupitia akaunti ya X alisema wawili hao, Bob Nyagi na Nicholas Ayoo 'walitekwa nyara na maafisa waliokuwa wamejihami' wakiwa kwenye kituo cha mafuta na kupelekwa kusikojulikana.

Hata hivyo, msemaji wa polisi Uganda, Kituma Rusoke ameiambia BBC kwamba wanaharakati hao wawili wa Kenya hawako chini ya ulinzi wa polisi.

"Watu hao [Bob Nyagi na Nicholas Ayoo] hawako chini ya ulinzi wa polisi, wasiliana na chombo kingine chochote [shirika la usalama]"

Alipotafutwa na BBC, msemaji wa jeshi Felix Kulayigye alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu ni madai yanayowahusisha ‘watendaji wa usalama’ wasio na sare.

Pia alimpa Bobi Wine jukumu la kuthibitisha madai ya utekaji nyara na ni chombo gani cha usalama kiliyaendesha.

"Katika sheria wanasema, uthibitisho upo kwa mshitaki" alisema.

Lakini mashirika ya usalama ya Uganda mara nyingi yamekuwa yakishutumiwa kwa kupanga kukamatwa kwa wanasiasa na wafuasi wa upinzani huku wakiwa hawajavaa sare.

Baadhi mara nyingi hujitokeza tena mahakamani kwa mashtaka ya jinai.

Wakati huo huo kampeni za urais zinaendelea katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Bob na Nicholas walikuwa wameshiriki hivi karibuni katika mikutano ya kampeni ya Bobi Wine, ambaye anatafuta kumng'oa rais aliye madarakani Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa takribani miongo minne.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI