Header Ads Widget

MAAMBUKIZI YA COVID YAONGEZEKA KUTOKANA NA AINA MPYA: NIMBUS NA STRATUS

 

Baadhi ya fedha hizo zitatumiwa kwa ununuzi wa vifaa vya kupima corona

Ikiwa unasumbuliwa na koo linalouma sana pamoja na homa, huenda umeambukizwa mojawapo ya aina mpya za virusi vya Covid-19 vinavyoenea kwa kasi msimu huu wa vuli.

Kwa mujibu wa mamlaka za afya nchini Uingereza, aina mpya za virusi—XFG (inayojulikana pia kama Stratus) na NB.1.8.1 (ijulikanayo kama Nimbus) ndizo zinazoongoza kwa kusababisha maambukizi kwa sasa.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa, kwa sasa, hakuna ushahidi kwamba aina hizi mpya ni hatari zaidi au husababisha madhara makubwa zaidi kiafya kuliko aina zilizopita.

Hata hivyo, mabadiliko ya kimaumbile yaliyojitokeza kwenye virusi hivi yanaweza kuongeza uwezekano wa kuambukiza kwa urahisi zaidi.

Dalili zinazojitokeza

Virusi hubadilika tabia zao kadri vinavyosambaa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

Mabadiliko hayo, yanapofikia kiwango fulani, husababisha kuibuka kwa “aina mpya” au variants.

Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa baadhi ya dalili zinazojitokeza sana katika maambukizi ya sasa ni pamoja na sauti ya kukwaruza na koo linalouma vikali kana kwamba limechomwa kwa wembe.

Hata hivyo, Covid-19 bado inaweza kusababisha dalili nyingi kama vile:

• Maumivu ya kichwa

• Kikohozi

• Pua kuziba au kutoa kamasi

• Uchovu wa mwili

Dalili hizi hufanana sana na zile za mafua ya kawaida au homa ya msimu, hivyo si rahisi kutambua tofauti bila kipimo rasmi.

Tahadhari na Ushauri wa Kiafya

Iwapo unahisi kuwa hujisikii vizuri na una dalili za Covid, ni vema kuepuka kukaribiana na watu walio katika hatari zaidi, kama wazee au watu wenye maradhi sugu.

Kukaa nyumbani inapowezekana pia kunashauriwa ili kuzuia kusambaza maambukizi zaidi.

Unapolazimika kutoka, vaa barakoa, osha mikono mara kwa mara, na tumia vitambaa safi (tishu) unapokohoa au kupiga chafya, kisha vitupe kwa usafi.

Hatua hizi husaidia kupunguza kuenea kwa Covid na magonjwa mengine ya njia ya hewa.

Kwa koo linalouma, unywaji wa maji ya kutosha na kijiko cha asali kunaweza kupunguza maumivu, kwa mujibu wa ushauri wa Huduma ya Afya ya Taifa (NHS) ya Uingereza.

Kwa mujibu wa Chuo cha Madaktari wa Familia nchini Uingereza (Royal College of General Practitioners), kiwango cha maambukizi ya Covid-19 kimeongezeka nchini kote, hasa miongoni mwa watoto wadogo na watu wazee.

Aidha, idadi ya wagonjwa wa Covid wanaolazwa hospitalini inaendelea kuongezeka, hali inayozusha hofu ya athari kubwa zaidi wakati wa msimu wa baridi.

Watu wenye umri wa miaka 75 na zaidi wanastahili kupata chanjo ya bure ya Covid kupitia NHS.

Kwa mujibu wa Shirika la Usalama wa Afya Uingereza (UKHSA), chanjo hizi bado zinatoa ulinzi mzuri hata dhidi ya aina mpya za virusi.

UKHSA inahimiza watu kupata pia chanjo dhidi ya mafua na virusi vingine vya baridi kama RSV (respiratory syncytial virus), ambavyo navyo huenea zaidi wakati wa majira ya baridi.

“Ni kawaida kwa virusi kubadilika. Kadri tunavyokusanya takwimu zaidi kuhusu aina hizi mpya, ndivyo tutakavyoweza kuelewa vyema jinsi vinavyoshirikiana na kinga ya mwili, na kuchukua hatua sahihi kulinda walio hatarini zaidi,” imeeleza UKHSA.

“Jambo muhimu zaidi ni kwa wale waliostahili kupokea chanjo, kuhakikisha wanafanya hivyo mara tu inapopatikana.” Dkt. Alex Allen, mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza UKHSA, amesema: “Kwa sasa, hakuna ushahidi kwamba aina hizi mpya husababisha maradhi makali zaidi, wala chanjo zinazotumika sasa kuwa na ufanisi mdogo dhidi yao.”

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI