NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Labani Kihongosi, amekutana na makundi mbalimbali ya wananchi Jijini Mwanza kutoa taarifa ya maendeleo ya kampeni za mgombea wa urais wa chama hicho.
Mkutano huo umefanyika leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu Jijini Mwanza. Kihongosi amesema kuwa kampeni za chama hicho zianzia Agosti 28, 2025 kwenye viwanja vya Tanganyika Packers Kawe, Jijini Dar es Salaam, na kesho zitakamilisha mwezi wa pili wa kampeni za kitaifa.
"Kati ya mikutano yetu ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025, tumefanikisha mahudhurio makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini. Takriban watu milioni 25.3 wamehudhuria mikutano ya hadhara, wakati watu milioni 57.1 wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ndani na nje ya nchi. Vilevile, mgombea wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefuatiliwa mara 164.9 milioni kupitia majukwaa mbalimbali ya mitandao," amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa amefurahia ushiriki mkubwa wa wananchi, na teknolojia ya mawasiliano imewezesha kufikia watu wengi zaidi kupitia redio, televisheni, magazeti, mitandao ya simu na kompyuta, pamoja na mabango barabarani na vibanda umiza. "Tumefanikisha kufikia Watanzania wengi kwa njia ambayo haijawahi kutokea," amesema.
Kihongosi pia amebainisha kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mikutano 112 na mikutano yote imekuwa na mafanikio makubwa. Katika baadhi ya maeneo, msafara wake umezuiliwa na umati wa wananchi, na hivyo kulazimika kuzungumza akiwa ndani ya gari. Wingi wa wananchi unaonyesha imani kubwa kwa CCM na upendo kwa mgombea huyo kutokana na uongozi wake unaojali wananchi.
Aidha, mgombea wa urais wa CCM siyo tu alieleza Ilani ya chama bali pia aliwasikiliza wananchi, hatua ambayo imesaidia kuhuisha ahadi zake kwa muhula ujao. Kihongosi amesema, "Mgombea wetu amefanya kazi kubwa katika kuinadi Ilani ya CCM. Tuna uhakika Watanzania wameielewa na wengi wako tayari kuchagua CCM kwa sababu Ilani yetu ni bora zaidi, na chama chetu ndicho kimebeba matumaini ya kweli ya wananchi."





0 Comments