.
Na Moses Ng’wat, Songwe.
Timu ya soka ya Iyula kutoka Wilayani Mbozi imeibuka bingwa wa Bonanza la Ushirika Cup Songwe, baada ya kuifunga timu ya Mwenge FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Oktoba 16, 2025, katika uwanja wa CCM Vwawa, Wilayani Mbozi.
Mashindano hayo, yaliyoandaliwa na Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Songwe (SORECU), yalilenga kuhusisha michezo pamoja na kutoa elimu kwa vijana juu ya matumizi ya nishati safi na umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika.
Mchezo wa fainali uliofanyika Oktoba 16, 2025, ulichanganywa na mchezo wa kuamua mshindi wa tatu, uliowakutanisha timu za Mpapa ya Wilayani Momba dhidi ya Magamba ya Wilayani Songwe, ambapo Mpapa walishinda 1-0.
Jofrey Yunji, Mratibu wa Bonanza na Ofisa Tehama na Michezo wa SORECU, alisema mashindano hayo yalianzia ngazi ya Wilaya kabla ya mabingwa hao wa wilaya kukutana katika fainali za Bonanza hilo.
Tawala msaidizi wa Mkoa wa Songwe anayesimamia Uchumi na Uzalishaji, Vansca Kulanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Jabiri Omary Makame, alikabidhi zawadi ya shilingi milioni 1 kwa mshindi timu ya Iyula.
Pia Kulanga alikabidhi zawadi ya shilingi 700,000 kwa mshindi wa pili, timu ya Mwenge kutoka Wilayani Ileje, huku timu ya Mpapa kutoka Wilayani Momba ikipokea shilingi 500,000 kwa nafasi ya tatu.
Kulanga alitumia fursa hiyo kufikisha ujumbe wa mkuu wa mkoa, akisisitiza umuhimu wa mabonanza ya michezo ili kuhamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa Oktoba 29.
Alisisitiza pia kuwa vijana, mbali na michezo, wanapaswa kushiriki katika kilimo, vyama vya ushirika, na uhifadhi wa mazingira.
Mwisho.
0 Comments