Askofu Mkuu na Muasisi wa Makanisa ya Bethel Calvary nchini Tanzania Baba Askofu Dkt. Willy Akyoo amesema amani ni daraja la Haki kwenye Jamii, akisisitiza kila mmoja kuilinda kwa maslahi ya maendeleo, haki na ustawi wa Jamii.
Baba Askofu Akyoo amebainisha hayo wakati alipozungumza na wanahabari Meru Mkoani Arusha kuhusu amani kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 akisisitiza kuwa hakuna uwezekano wa kupata maelewano ama haki yoyote ile kwenye jamii pasipokuwa na amani ambayo inawezesha mifumo ya kisheria na kijamii kuweza kufanya kazi katika utaratibu ufaao kwenye kumuhudumia Mtanzania.
"Umuhimu wa amani kwa Tanzania limekuwa na mjadala mkubwa wengi wakisema hakuna amani bila haki na wengine wakikariri kuwa amani ni tunda la haki, mimi siamini hivyo mimi naamini amani ni daraja la kwenda kwenye haki, kwamba amani ikiwepo ndiyo itakayotoa mazingira sahihi ya haki kupatikana. Hakuna uwezekano wa kupata haki kama hakuna amani kwasababu aliyeshikilia haki yako ni vipi utaipata haki hiyo ikiwa utaondoa amani kwenye meza ya mazungumzo? Amekaririwa akisema Askofu Akyoo.
Akirejea maandiko matakatifu kwenye Kitabu cha Biblia, Baba Askofu Akyoo ameeleza kuwa Vitabu vya dini vinaagiza kuitafuta amani kwa bidii na kwa watu wote, akiwataka Vijana kutokubali kutumika katika kuharibu ba kuratibu shughuli ama matendo yoyote ya uvunjifu wa amani, akiwataka kulinda hatma zao.
Aidha Askofu Akyoo ameeleza pia kuhusu umuhimu wa kupiga kura kwa Vijana, akisema kupiga kura ni mwanzo wa Vijana kuitawala nchi yao na kutafuta majawabu ya changamoto zao, akihamasisha kila mmoja mwenye haki na sifa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 ili kuwachagua Viongozi wenye kuweza kuwaletea maendeleo na kulinda amani na hatma za maisha yao.
0 Comments