Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bariadi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Kundo Mathew amewataka wananchi kumchagua Mgombea Urais Dk. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuleta Maendeleo na kwamba baada ya uchaguzi, serikali itakamilisha usambazaji wa Umeme kupitia Mradi wa Compact 300.
Amesema kuwa mradi huo utatekelezwa Mahususi kwa ajili ya kata za Mji wa Bariadi ili kuondokana na changamoto ya nguzo za Umeme na Mradi huo utafikisha huduma hiyo muhimu kwa Wananchi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza kwenye mikutano ya Kampeni iliyofanyika Mitaa ya Nkuli (kata ya Guduwi) na Mwakibuga (kata ya Nyakabindi), Mhandisi Kundo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi wa CCM ili waweze kutekeleza miradi ya Maendeleo ikiwemo Umeme, Maji na Barabara.
Amesema kuwa Dk. Samia ndie Mgombea wa nafasi ya Urais mwenye sifa za kuendelea kuwa Rais, huku akiwasisitiza kuchagua viongozi watakaowaletea Maendeleo akiwemo yeye Mbunge (Mhandisi Kundo) pamoja na Madiwani wa CCM.

"Tuna Mitaa minne haina Umeme katika Jimbo la Bariadi mjini, kwa dhamira ya Dk. Samia, tunaenda kutekeleza kuleta Umeme katika Mitaa hiyo kupitia Mradi wa Compact Mission 300, tutamwaga nguzo ili kuwafikishia huduma wananchi ikiwemo Mtaa wa Nkuli" amesema na kuongeza.
"Umeme ndio Uchumi na ajira kwa vijana ambao watajipatia kipato na uchumi utaimarika...Umeme ni Uchumi, Umeme ni mawasiliano, tuchagueni viongozi tunaojua matatizo yenu, tuchagueni kwa sifa za Uongozi, Kura yako sauti yako, sauti yako ndio Maendeleo".
Mhandisi Kundo amesema kuwa endapo atachaguliwa Oktoba 29, 2025, atahakikisha anaimarisha Barabara pamoja na kuweka taa za Barabarani kwenye mtaa wa Mwakibuga ili Wakina mama wafanye Biashara mpaka usiku.
Amesema kuwa agenda ya CCM ni kutatua changamoto za wananchi na kwamba wameandaa Ilani ya kuchochea Mapinduzi ya kisasa kupitia sayansi na teknolojia, kuimarisha mawasiliano na sekta ya Afya ili wananchi wasipate changamoto.
Mwisho.
0 Comments