Header Ads Widget

MADIWANI MANISPAA MOROGORO WAMLALAMIKIA KATIBU WA CCM(W) KWA VITENDO VYA UBAGUZI

 

Na Matukio DaimaAPP

BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wamelalamikia vitendo vya ubaguzi wa jinsia na ukabila unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama ngazi ya Wilaya.

Tuhuma hizo zimetolewa na baadhi ya madiwani kufuatia vitendo na matukio yaliyojitokeza wakati wa kampeni na uchaguzi wa Meya na naibu Meya uliofanyika Desemba Mosi Mwaka huu.


Madiwani hao ambao hawakutaka majina yao kuandika walisema, katibu wa CCM Wilaya Twahib Berege alikuwa akiongoza waziwazi kampeni zilizoonyesha ubaguzi wa jinsia na ukabila, ambapo alitaka viongozi wa nafasi hizo watokane na jinsia ya kiume na kabila la watu wa Morogoro.


"Ni kweli Berege ni kiongozi wetu wa chama lakini alishiriki kuhamasisha baadhi ya madiwani kumchagua naibu meya ambaye ni mzawa wa Morogoro na kwamba,"alisema diwani huyo ambaye hakutaka kutajwa.


Mmoja wa wagombea wa nafasi ya naibu Meya Latifa Ganzel alipozungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tuhuma hizo alikiri kuwa ni kweli Katibu huyo Berege alifanya kampeni zisizofaa dhidi yake na kwamba alifikisha malalamiko yake kwa katibu wa Ccm mkoa pamoja na mwenyekiti wa Ccm wilaya Fikiri Juma.


Hata hivyo uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa nafasi zote za juu za uongozi wa Baraza la madiwani halmashauri ya manispaa ya Morogoro zinashikiliwa na jinsia moja pekee


Nafasi hizo ni pamoja na Meya  Naibu meya pamoja na wenyeviti wa kamati zote.


Baadhi ya madiwani wanawake walisema katibu huyo alikuwa akifanya kampeni za kumtaka naibu meya  wa jinsia fulani na kwamba aliwaeleza kuwa hakuna Imamu Mwanamke,alisema mmoja wa madiwani hao ambaye hakutaka jina lake litajwe.


Madiwani hao walisema kufuatia kuendesha kampeni hizo dhidi ya mgombea unaibu meya mwanamke ambaye ni Latifa Ganzel, katibu wa Jumuiya ya wanawake Judithi Laiza aliwaita madiwani wanawake na kuwataka kumuunga mkono mwanamke huyo ili kuleta usawa kwenye uongozi.


Katibu wa CCM Wilaya ya Morogoro mjini Twalib Berege alipotafutwa juu kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo alisema, tuhuma hizo si za kweli na wanaolalamika ni wale ambao walishindwa na wanafuta uhalali wa kushindwa kwao.


Alisema "Siku zote unaposhindwa ukubali,watu wanaothibitishwa kushindwa kwao wamekuwa wakijaribu kusema lolote,".


Berege pia alisema kwa Sasa wanaangaika na uchaguzi wa kata ambazo hazikufanya uchaguzi na kwamba kikao Cha uteuzi wa katibu wa madiwani kitakaa wakati wowote baada ya uchaguzi wa kata.


"Tarehe 30 Desemba 2025 na Januari 5,2026 ndo tunatarajia kufanya chaguzi kwenye hizo Kata,"alisema katibu wa Wilaya Berege.


Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro Nuru Ngereja akizungumza kwa njia ya simu alisema wanaojitangaza kuwa tayari wamepitishwa kuwa katibu wa madiwani hawajiamini na hawafai kuwa viongozi.


"Hao Wanaojitangaza hawajiamini na hawafai kuwa viongozi ndio sababu wanadai kusimamiwa na viongozi wa juu ili wasipate ushindani,"alisema Ngereja.


Katibu huyo alisema hadi sasa hakuna maelekezo yoyote yaliyotolewa kwa ajili ya kumpata katibu wa madiwani.


Ngereja alisema katibu wa madiwani kawaida anateuliwa na madiwani wenyewe miongoni mwao na chama jukumu lake ni kutoa maelekezo jinsi ya kumpata katibu wao 


Ngereja alikuwa akitoa ufafanuzi juu ya  malamiko ya baadhi madiwani wa halmashauri ya  manispaa ya Morogoro kudai kuna ambao wanatamba kuwa tayari nafasi hiyo ni yao kwa sababu wanakubalika kwa viongozi wa chama.


Malalamiko mengine ni ubaguzi wa jinsia na ukabila ndani ya baraza hilo pamoja na makundi yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa meya na naibu meya.


Mwisho.

Post a Comment

0 Comments



MAGAZETI



NAMBA ZA HUDUMA YA USAFIRI WA KUKODI